Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson,akikabidhiwa fomu ya kuwania nafasi ya USPIKA wa Bunge,na Katibu msaidizi Mkuu Idara ya Organaizesheni Bw. Solomon Itunda katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma leo Januari 10,2022.
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog-DODOMA.
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Dk.Tulia Akson leo amechukua fomu ya kuwania kiti cha Spika wa Bunge hilo ambayo imeachwa wazi na Job Ndugai aliyetangaza kujiuzulu nafasi hiyo hivi karibuni.
Akiongea mara baada ya kukabidhi fomu hiyo kwa Katibu msaidizi Mkuu, Idara ya Organaizesheni Solomon Itunda katika Ofisi za Makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi Dodoma, Dk.Akson amesema kuwa amefikia uamuzi huo kwa kuwa ana uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge na kusisitiza kuwa atahakikisha anasimamia misingi ya kusimamia sheria na kanuni za bunge ikiwa atapata nafasi hiyo.
Kuhusu utendaji wa aliyekuwa Spika wa Bunge hilo ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (Ndugai),Dk.Tulia amesema kuwa aliongoza Bunge vizuri na kwamba hakuna kilichopwaya kwa kipindi chote alichokuwepo kwenye nafasi hiyo.
"Ndugai aliendesha shughuli za Bunge vizuri na wala hakupwaya, nitaendelea kusimamia misingi ya haki pamoja na kuliweka bunge karibu na serikali kwa malengo ya pamoja ya kupata maendeleo kwa wananchi",amesema
Ameeleza kuwa ikiwa atapata nafasi ya kuwa Spika atahakikisha misingi yote ya kibunge inazingatiwa,sheria na kanuni za bunge zinalindwa pamoja na kutoa haki kwa wabunge wote.
"Tutafanya kazi ya kutunga sheria ,kuishauri serikali pamoja na kuhakikisha serikali na bunge linakuwa na ushirikiano wa kutosha ili kuharakisha maendeleo",amesema Tulia.
Kuhusu nafasi yake ya unaibu Spika amesema kwa sasa bado ipo pale pale kwani katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawataja watu ambao hawaruhusiwi kugombea kuwa ni Waziri mkuu Mawaziri na Manaibu Makatibu wakuu.
"Mimi sina kizuizi hivyo nafasi yangu bado ipo pale pale ,"amefafanua Dk.Tulia.
Social Plugin