MTU mmoja miongoni mwa majeruhi wanane waliolazwa katika Hospitali ya Ndanda kwa ajali ya gari waliokuwa kwenye ngoma ya unyago mkoani Mtwara, amefariki dunia na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kufikia 15.
Ajali hiyo ilitokea Januari 2 mwaka huu katika Kijiji cha Lidumbe Wilaya ya Newala mkoani humo ambapo jumla ya watu 22 walijeruhiwa katika ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njera alisema jana kuwa mtu huyo aliyefariki dunia akiwa hospitalini amelazwa baada ya kujeruhiwa kwenye ajali hiyo iliyotokea saa 2:00 usiku katika Kijiji cha Lidumbe wilayani Newala, ni Hawa Hashimu (22).
Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 622 AFS ambapo lilikuwa katika mwendokasi likitokea Newala kuelekea Mji mdogo wa Mahuta Tandahimba na kuwagonga wakazi wa kijiji hicho wakiwa katika sherehe hiyo.
Kati ya majeruhi 22, majeruhi 14 waliendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo ya Newala na wengine wanane walifikishwa Hospitali ya Ndanda wilayani Masasi mkoani humo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Majeruhi mmoja aliyelazwa kwenye hospitali hiyo ya wilaya, Atari Idrisa (13) ambaye ni mwanafunzi ameruhusiwa baada ya hali yake kuimarika na wengine bado wanaendelea na matibabu katika hospitali hizo ikiwemo hiyo ya Newala pamoja na Ndanda.
Wengine waliokufa katika ajali hiyo ni Ahmadi Nampande (32), Hakifalu Juma (10), Rashida Salumu (25), Hawa Ramadhani (33), Hassara Hamza (27), Salima Jafari (28), Rashidi Bakari (38), Raia Shabani (04), Shakira Seifu (35), Gadafi Ally (27), Shiru Hussen (29), Avila’s Selemani (24), Zuhura Kasimu (20), Masudi Abdul (24).
Social Plugin