Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Tanzania iko mikononi mwa Mungu na ndiyo maana imeendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu na kimbilio la mataifa yaliyopoteza tumaini.
Kauli hiyo ameitoa jimboni kwake Ruangwa mkoani Lindi, akiwa kwenye mapumziko yake ya mwisho wa mwaka, na kusema kwamba serikali za awamu zote zimeendelea kuheshimu uwepo wa dini nchini kwani miongozo na mafundisho yanayotolewa na viongozi wa dini mbalimbali yanawafanya waumini wao kuwa raia wema.
"Nchi hii imeshikwa na Mwenyezi Mungu na ni kwa sababu viongozi wa dini wanaendelea kuliombea Taifa hili, kwa hiyo na sisi tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba nchi hii inabaki kwa salama," amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewataka Watanzania wampe nafasi Rais Samia ya kufanya kazi kwa sababu amekuwa serikalini kwa muda mrefu na anajua ni nini Watanzania wanatamani serikali yao iwafanyie na kusema madaraka yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu na yeye ndiye hupanga nani awe nani na kwa wakati gani.
“Kila nafasi imetengenezwa na Mwenyezi Mungu na kila anayekwenda kuongoza Mwenyezi ndiye amesema wewe utakuwa pale, na kama hajasema, hutokuwa, utatumia hela nyingi na zitapotea bure, utakwenda na mambo mengine ya giza, lakini hutomudu, Mungu keshasema huyu ni huyu, tuwaheshimu walioko kwenye nafasi za kuwatumikia Watanzania wafanye kazi zao kwa weledi,”ameongeza.
Chanzo- EATV
Social Plugin