Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuchambua matukio yote ya ajali za barabarani kwenye misafara ya viongozi nchini ambayo yanachukua maisha ya wana tasnia hiyo.
Amesema hayo wakati akitoa pole kwenye hafla ya kuaga miili ya wanahabari watano mkoani Mwanza.
"Nilipokuwa nakuja huku wakubwa wangu wamenielekeza kuwa nifuatilie hili la ajali kwenye misafara ya viongozi,kwanini waathirika wamekuwa ni waandishi wa habari,lazima tujue chanzo ni nini?",amesema.
Waziri Nape amesema baada ya kukabidhiwa taarifa ya uchunguzi mambo mengine yatafuata ikiwemo kubadilisha utaratibu mzima.
Amesema utaandaliwa utaratibu maalumu au itifaki rasmi ya namna bora ya ushiriki wa wanahabari kwenye ziara hizo.
Kauli hiyo ya Nape imejibu kilio cha Wanahabari wengi nchini kuwa mara nyingi hawapewi kipaumbele kwenye ziara hizo, ambapo mara nyingi wanapewa magari yasiyo na viwango, ambayo hayawezi kuendana na mwendo wa misafara yenyewe na kujikuta yakiachwa nyuma na pale wanapojitahidi kukimbia ili kuwahi matukuio wanaishia kupata ajali na kupoteza maisha
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye akizungumza mbele ya Wombolezaji waliofika kuaga miili ya wanahabari watano katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel (kushoto) akimpa salamu za Pole Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (kulia) wakati wa shughuli ya kitaifa ya kuaga miili ya waandishi wa habari watano waliofariki kwenye ajali ya gari iliyotoea katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Robert Gabriel akielekea Wilaya ya Ukerewe jana Januari 11,2022.
Wa pili kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Molle,kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagina Wombolezaji wengine wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri uwanjani hapo wakati wa shughuli ya kuaga miili ya Waandishi wa Habari watano waliofariki kwenye ajali hapo jana mkoani Simiyu.