Na Dotto Kwilasa,Dodoma
ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa Asia Abdallah amechukua fomu ya kugombea Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akidai sababu ni kutaka kumuunga mkono kwa vitendo Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wake.
Asia anaungana na wanachama wengine 30 wa CCM ambao mpaka leo wamechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma mara baada ya kuchukua fomu,Asia amesema sababu iliyomsukuma kuchukua fomu ni kuvutiwa na uongozi wa Rais Samia kwa sababu ameitetea Nchi hivyo hana sababu ya kuacha kumuunga mkono akiwa ndani ya mfumo na nje ya mfumo.
“Nimevutiwa na uongozi wa Rais wetu kwa sababu anafanya kazi anaitetea Nchi tumepita katika hatua ngumu ameweza kuisimamia Nchi imetulia na mimi kiukweli ninakila sababu ya kumuunga mkono kwa namna yoyote ile ndani ama nje ya mfumo,”amesema.
Amesema amechukua fomu kama Katiba inavyoelekeza kwamba mtu yeyote anaweza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uspika na amejipima ameona anatosha na atashirikiana na Wabunge na wananchi pamoja na mihimili ningine Mahakama na Serikali.
“Nimechukua fomu kama katiba ambavyo inaelekeza mtu yeyote anaweza kuchukua fomu kugombea uspika na mimi pia nimeona nina kila sababu nia ipo nimechukua fomu ili niweze kushirikiana na Wabunge na wananchi na mihimili mingine Mahakama na Serikali ili tuweze kujenga Taifa letu.
“Na mimi ninachokiona huu ni mhimili kati ya ile mitatu mimi naona nikiwa kiongozi wa mhimili huo kazi yangu ni kufanya majukumu ya huo mhimili kufuata kanuni na taratibu na sheria zote bila kuisahau katiba ya Nchi.
“Kikubwa ni kufanya kazi kama timu kwa sababu wote lengo ni moja tunajenga Nchi moja tumsaidie Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu,”amesema Asia.
Wengine waliochukua fomu leo Makao Makuu ya CCM Dodoma ni pamoja na Dk. Musa Ngonyani,Faraji Rushagama,Hamisi Rajabu na Dk.Titus Kamani huku kwa upande wa Ofisi ndogo za Lumumba Jijini Dar es Salaam waliochukua fomu ni pamoja na Festo Kipate,George Nangale,Baruan Mwakilanga,Zahoro Hanuna.
Wengine ni Mwanasiasa mkongwe nchini Andrew Chenge,Thomas Kirumbuyo na Angelina John huku kwa upande wa Afisi Kuu Zanzibar aliyechukua fomu ni Eng. Abdulaziz Jaad Hussein.