MWANAMME mmoja mwenye umri wa miaka 45 amemuua mke wake na wanawe watatu kabla ya kuteketeza kwa kuichoma moto nyumba yao katika Kijiji cha Kahua, Kapsita katika Kaunti ndogo ya Molo nchini Kenya.
Akithibitisha kisa hicho, Kamishna wa Kaunti ndogo ya Molo, Josephat Mutisya amesema kuwa mwanamme huyo aliteketeza nyumba yao baada ya kutekeleza mauaji hayo. Polisi walipokea ripoti kuwa nyumba moja ilikuwa ikiteketea, baada ya kufika eneo la tukio walimkuta mshukiwa huyo, akipiga mayowe ya msaada.
“Tulipokea taarifa ilikuwa majira ya saa sita usiku kuwa kuna nyumba inayoteketea. Polisi walipofika eneo la tukio walimkuta mwanamme akipiga makelele kuomba msaada nje ya nyumba hiyo. Mwanamme huyo ndiye mshukiwa,” Mutisya alisema.
Jirani mmoja kwa jina Newton Ratemo ambaye alizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa walishindwa kuingilia na kuokoa wanne hao kwani nyumba hiyo ilianza kuteketea na kuwafanya kuitisha msaada wa maafisa wa polisi.
Naibu Kamishna huyo alisema kuwa mkasa huo ulitokana na mzozo kati ya mwanamme huyo na mkewe. Afande Mutisya amewataka wananchi kutafuta njia mwafaka za kutatua mizozo badala ya kuchukua sheria mikononi mwao.
“Ni mawazo ya kuhangaisha yaliyomfanya mwanamme huyo kuteketeza nyumba yake mkewe na wanawe watatu wakiwa ndani. Ninatoa wito kwa wakaazi kuzungumza kuhusu matatizo yao yanayowasibu nyumbani. Zungumza na jamaa, viongozi wa kidini na watu wengine wa usaidizi,” alisema Mutisya.
Social Plugin