WAZIRI wa Maji,Jumaa Aweso,akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa Bodi za Maji za Mabonde hafla iliyofanyika leo Januari 21,2022 jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji Bi.Wanyenda Kutta,akitoa maneno mafupi kuhusu makabidhiano ya Magari wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa Bodi za Maji za Mabonde hafla iliyofanyika leo Januari 21,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Rasiliamali za Maji Dk.George Lugomela,akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa Bodi za Maji za Mabonde hafla iliyofanyika leo Januari 21,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugani kutoka Wizara ya Maji Dk.Christopher Nditi,akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa Bodi za Maji za Mabonde hafla iliyofanyika leo Januari 21,2022 jijini Dodoma.
Wakurugenzi wa Wizara ya Maji na Wakuu wa Vitengo pamoja na Maafisa Maji wa Bodi za Maji za Mabonde na wawakilishi wakifatilia hotuba ya Waziri wa Maji,Jumaa Aweso,(hayupo pichani ) wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa Bodi za Maji za Mabonde hafla iliyofanyika leo Januari 21,2022 jijini Dodoma.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso,akikabidhi funguo kwa Maafisa wa Maji mara baada ya kukabidhi magari kwa Bodi za Maji za Mabonde hafla iliyofanyika leo Januari 21,2022 jijini Dodoma.
Waziri wa Maji,Jumaa Aweso,akimsiliza Mkurugenzi wa Bonde Ruvuma na Pwani ya Kusini Bw.Jumanne Mpemba ,akitoa neno la shukrani kwa niaba wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa Bodi za Maji za Mabonde hafla iliyofanyika leo Januari 21,2022 jijini Dodoma.
Muonekano wa Magari manne yaliyokabidhiwa kwa bodi za maji za Mabonde nchini
..........................................................
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Maji,Jumaa Aweso ametaka mikakati ya pamoja kati ya Bodi za maji za mabonde nchini na Halmashauri za Wilaya kutatua changamoto za maeneo yenye changamoto ya ukosefu wa maji,au yanayokumbwa na ukame wa mara kwa mara.
Ameitaja mikakati hiyo ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa mabwawa na malambo nchini kote.
Akizungumza leo Januari 21,2022 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi magari kwa bodi za maji za Mabonde nchini,Waziri Aweso amesema hivi karibuni kumekuwepo na upungufu mkubwa wa maji katika vyanzo vingi vya maji na kusababisha adha ya ukosefu wa maji kwa ajili ya binadamu, mifugo na uzalishaji.
Amesema hali hiyo ilitokana na kutokunyesha au kuchelewa kwa mvua za vuli, kutokusimamia vyema matumizi ya maji na vibali vinavyotolewa, lakini pia kutokuwekeza katika miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua,pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Kutokana na hili, ninazitaka Bodi zote za Maji za Mabonde kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, kutambua maeneo yote yenye changamoto kubwa ya ukosefu wa maji au yanayokumbwa na ukame wa mara kwa mara na kukosa maji kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
“Ikiwa ni pamoja na mifugo na kilimo, na tuweke mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa mabwawa na malambo nchini kote,”amesema.
Aidha, amesema kumekuwa na utaratibu wa kila sekta kujipangia na kujijengea miundombinu ya maji kama visima, mabwawa na malambo bila kushirikiana.
“Ambapo utakuta eneo moja lina miradi mingi ya visima/mabwawa kwa ajili ya shughuli hizo za kisekta wakati maeneo mengine hakuna jitihada zozote zimechukuliwa.
“Kumbe tungekuwa tumeweka nguzu zetu wote pamoja ama kushirikiana, badala ya eneo moja kuwa na malambo matatu, basi maeneo mengine kadhaa yangekuwa na huduma hiyo,”amesema
Amesema kutokana na hilo,amemuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali za Maji, kuratibu ushirikiano wa karibu wa Sekta nne za Maji, Mifugo, Uvuvi na Kilimo ili kwa pamoja ziweze kuoanisha mipango.
Katika hatua nyingine,Aweso amezikumbusha Bodi za maji za mabonde nchini kufanya tathmini za uhakika za rasilimali za maji nchini pamoja na kuweka mikakati ya kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji nchini.
Pia,ameagiza Bodi za Maji za Mabonde kufanya zoezi la utambuzi wa watumia maji wote ikiwa ni pamoja na kuwasajali na kusimamia zoezi la ukusanyaji wa maduhuli ya matumizi ya maji na vyanzo vingine vya mapato kwa ufanisi mkubwa ili waweze kuongeza mapato ya Bonde.
Waziri Aweso amezitaka ,kudhibiti na kuzuia uchafuzi wa vyanzo vya maji, kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kusimamia matumizi sahihi na yenye ufanisi ya maji.
Vilevile, kushiriki na kulinda maslahi, hadhi, udugu na ujirani mwema katika usimamizi wa rasilimali za majishirikishi,kutekeleza mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
“Pamoja na kukamilisha mipango hiyo katika Mabonde ya Ziwa Victoria na Pangani; na kuongeza ushiriki wa wadau mbalimbali katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
Waziri Aweso amesema Wizara imetumia fedha nyingi na jitihada kubwa katika kuhakikisha mazingira ya kiutendaji ya Bodi za Maji za Mabonde yameboreshwa.
“Jitihada hizi ni kama mbegu zilizosiwa ardhini ambapo mwishoni tunategemea ziote na kutoa mazao.
Aidha,Waziri Aweso ameagiza Bodi za Maji za Mabonde kufanya zoezi la utambuzi wa watumia maji wote ikiwa ni pamoja na kuwasajali na kusimamia zoezi la ukusanyaji wa maduhuli ya matumizi ya maji na vyanzo vingine vya mapato kwa ufanisi mkubwa.
“Ili kuongeza mapato ya Bonde na hatimaye, muweze kujiendesha na kutekeleza majukumu yenu ya kila siku, zikiwemo pia shughuli za maendeleo ya mabonde yenu,”amesema.
Vilevile,Aweso ameiagiza bodi hiyo kuyatunza magari haya kwa bidii kubwa na kuyakabidhi kwa madereva makini ili yakadumu na kusaidia katika kutekeleza majukumu yenu.
“Ninawataka pia mkajipange vizuri zaidi na kurekebisha changamoto ama mapungufu yaliyokuwa yanasababishwa na ukosefu wa vifaa kazi kama magari ili mkaimarike zaidi kiutendaji,”amesema.
Amesema Wizara ya Maji ina jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
“Ukiachilia mbali jukumu la Wizara la kusambaza maji kwa ajili matumizi ya nyumbani, Wizara ina jukumu la kugawa maji kwa ajili ya matumizi ya sekta mbalimbali kama vile mifugo, uvuvi, uzalishaji wa umeme wa nguvu za maji, matumizi ya viwanda, kilimo cha umwagiliaji,”amesema.
Social Plugin