Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YATANGAZA PUNGUZO KUBWA LA RIBA LA HADI ASILIMIA 9

 

  
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wakati wa kutangaza punguzo kubwa la riba katika mikopo ya kundi la wakulima ambapo sasa ni asilimia 9, pamoja na wafanyakazi ambao sasa riba yao itakuwa ni asilimia 13, uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Benki hiyo yaliyopo Palm Beach, Dar es salaam leo. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRBD, Bruce Mwile (wa pili kulia), Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa. Nsekela amesema punguzo hilo la riba linakuja kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Benki Kuu kuhusu kupunguza riba za mabenki ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

 
Benki ya CRDB leo imetangaza punguzo kubwa la riba katika mikopo kwa kundi la wakulima, pamoja na wafanyakazi. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Makao Makuu ya benki hiyo yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema punguzo hilo la riba linakuja kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mabenki kuhusu kupunguza riba ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Nsekela amesema katika punguzo hilo, riba ya mikopo ya kilimo imepunguzwa hadi 9% kutoka 20% iliyokuwa ikitozwa hapo awali, huku riba ya mikopo ya wafanyakazi ikipunguzwa kutoka 16% hadi kufikia asilimia 13%. Punguzo hilo la riba, linatoa ahueni kwa wateja wa Benki ya CRDB kulipa mikopo yao kwa riba nafuu, viwango vya chini zaidi vya marejesho ya awali, pamoja na kupata wigo mpana wa kukopa.
 “Kwa ushirikiano mkubwa na Benki Kuu ya Tanzania ambae ndie msimamizi wa sekta ya benki nchini, mwishoni mwa mwaka jana tuliweza kukaa chini na kuanza utekelezaji wa mchakato wa kupitia upya riba za mikopo mbalimbali inayotolewa na Benki yetu na hivyo ninajivunia kuona leo hii tumekuja na suluhisho la kilio cha muda mrefu cha wateja wetu,” amesema Nsekela huku akiwahamasisha wateja na Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.

Kwa upande wa mikopo ya kilimo Nsekela amesema punguzo hilo la hadi 9% ni kubwa kupata kutokea katika soko, huku akibainisha kuwa benki hiyo imetoa punguzo hilo ili kusaidia kuimarisha sekta ya kilimo ambayo huchangia 26% ya pato la Taifa na kutoa ajira kwa 75% ya Watanzania. “Lengo letu ni kuchochea kasi ya mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini kwa kuwawezesha wakulima wadogo na wakati kufanya kilimo cha kisasa kupitia mikopo nafuu ya pembejeo na zana za kilimo,” amesema Nsekela.
Benki ya CRDB ndio inayoongoza nchini kwa kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo kwa kutoa asilimia 40 ya mikopo yote ya kilimo nchini. Punguzo hilo la riba katika mikopo ya kilimo inadhihirisha azma ya Benki hiyo katika kuunga juhudi za serikali za kuwaletea watanzania maendeleo kwa vitendo. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,  Benki ya CRDB imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi 1.6 trilioni kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani katika kilimo.

Akielezea punguzo la riba kwa mikopo ya wafanyakazi, Nsekela amesema benki hiyo imejipanga kuendelea kuboresha ustawi wa wafanyakazi nchini kupitia mikopo ya riba nafuu. “Wafanyakazi ni kundi muhimu kwa Benki yetu ndio maana tumekuwa tukiboresha kwenye riba ya mikopo ya kundi hili kila mwaka ili kuwasidia kufikia malengo waliyojiwekea jambo ambalo litaongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi,” amesema Nsekela. 
Nsekela amewataka wafanyakazi kuchangamkia fursa hiyo ya kushuka kwa riba kuimarisha kuboresha maisha yao kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, huku akiwaasa kutokopa bila ya kuwa na malengo. “Hii ni mara ya tatu ndani ya miaka mitano iliyopita kwa Benki yetu kupunguza riba ya mikopo ya wafanyakazi, matarajio yetu ni kuwa wafanyakazi watachangamkia fursa hii ili kuboresha maisha yao na hilo ndo haswa lengo la Benki ya CRDB.” 

“Viwango vikubwa katika tozo za mikopo imekuwa changamoto kwa watanzania wengi hasa wale wa daraja la kati na la chini lakini sasa tunaamini kuwa hata wale ambao hawakuweza kukopa sasa watatumia fursa hii kuboresha biashara zao na maisha yao kwa ujumla. Lakini pia tunaamini ndiyo maono hasa ya Mheshimiwa Rais kuona Watanzania wakishiriki kwa wingi katika shughuli za kiuchumi,” aliongeza Nsekela.
Kwa miezi kadhaa sasa Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imekuwa ikitoa wito kwa taasisi za fedha kupunguza riba kwa wateja ili kuimarisha uchumi. Kufanikisha hilo Benki Kuu imechukua hatua mbalimbali za kisera ikiwamo kupunguza kiwango cha sehemu ya amana za mabenki kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu, pamoja na kuanzisha mfuko maalum wenye thamani ya shilingi trilioni moja ambao utatumika kukopesha mabenki na taasisi za fedha kwa riba ya nafuu, ili ziweze kukopesha sekta binafsi.

Kwa mujibu wa Nsekela, hatua hizi mpya za Serikali zinasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi, kwa kuziwezesha benki nyingi kuwa na ukwasi wa kutosha kukopesha wateja kwa riba nafuu kama ambavyo imefanywa na Benki ya CRDB. Nsekela alimalizia kwa kusisitiza kuwa Benki ya CRDB itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali kupitia Benki Kuu ili kuhakikisha uchumi wa nchi unaimarika kupitia uwezeshaji wa sekta zote za maendeleo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com