Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YAZINDUA KAMPENI KUHAMASISHA WATANZANIA KUTUMIA HUDUMA NA BIDHAA BUNIFU CRDB



Benki ya CRDB imewataka Watanzania kutumia huduma na bidhaa bunifu zinazotolewa na benki hiyo kwa makundi mbalimbali ya wateja kufanikisha malengo waliyojiwekea katika mwaka huu mpya wa 2022. Hayo yamesemwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Unachostahili ni CRDB Bank” inayolenga katika kutoa elimu na kuwaonyesha Watanzania fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki yao ya CRDB


Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema Benki ya CRDB ikiwa benki ya kizalendo inatambua kuwa inawajibu wa kuwasaidia Watanzania na wadau wengine wa maendeleo nchini kutimiza malengo katika mwaka huu mpya 2022. Nsekela alisema kupitia kauli mbiu yake ya “Benki inayomsikiliza mteja”, Benki ya CRDB imekuwa ikisikiliza na kufanyia kazi mahitaji ya wateja ili kuwapa wanachostahili.
“Mwaka jana tulifanya utafiti maalum kufahamu mahitaji halisi ya wateja ambayo yamekuwa yakibadilika kila uchwao, utafiti ule ulienda sambamba na kupokea maoni ya namna bora ya kuwahudumia wateja. Ninajivunia kusema tumeweza kufanyia kazi maoni ya wateja na kuboresha sehemu kubwa ya huduma na bidhaa zetu ili kuweza kuwapa wanachostahili,” amesema Nsekela.


Nsekela alisema moja ya maeneo ambayo Benki hiyo imeyafanyia maboresho ni katika mtandao wa ufikishaji huduma za kibenki ambao unajumuisha mifumo ya kidijitali ikiwamo SimBanking, CRDB Wakala, TemboCard, na Internet banking ambayo inawawezesha wateja kupata huduma popote pale walipo. Hivi sasa wateja wa Benki ya CRDB wanaweza kupata zaidi ya asilimia 90 ya huduma kupitia njia hizo mbadala za upatikanaji wa huduma.
“Tunatambua wateja wanahitaji muda mwingi zaidi katika kufanya shughuli zao za kiuchumi, hivyo uboreshaji wa mifumo hii utawawezesha kufanya miamala yao kwa wakati na hivyo kuongeza ufanisi katika biashara na maeneo yao ya kazi hivyo kuongeza ufanisi,” amesema Nsekela huku akibainisha maboresho hayo yamesaidia kuongeza urahisi na unafuu wa kwa wateja.


Katika kampeni hiyo Benki ya CRDB pia imejipanga kuwaelimisha wateja juu ya huduma za uwezeshaji zinazotolewa na benki hiyo kupitia mikopo kwa makundi mbalimbali ya wateja ikiwamo wanafunzi, wafanyakazi, wajasiriamali, wakulima, wafanyabishara, makampuni na taasisi. “Niwahakikishie kuwa Benki yetu ina uwezo mkubwa kimtaji unaowezesha kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali kwa gharama nafuu, hivyo niwasihi Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kufikia malengo yao.”
Nsekela alisema benki hiyo pia imejipanga kuendelea kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati ya Serikali huku akimpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza utekelezaji wa miradi hiyo. “Ukubwa wa mizania yetu unatufanya tuwe na uwezo mkubwa wa kushiriki katika kuwezesha wadau wote wanaoshiriki katika miradi hii ikiwamo Serikali yenyewe, pamoja na wakandarasi na wazabuni,” amesema Nsekela.


Aidha, Nsekela alieleza kuwa katika kipindi cha kampeni hiyo wateja pia watakuwa wakielimishwa juu ya umuhimu wa kujiwekea akiba ili kufikia malengo kwa kutumia akaunti mbalimbali za benki hiyo. Benki ya CRDB ina akaunti zinazoongoza makundi mbalimbali ya wateja kuanzia akaunti za Junior Jumbo maalum ya watoto, wanafunzi - Scholar, wafanyakazi - Salary, wajasiriamali - Hodari, wafanyabiashara - Current, wakulima – FahariKilimo, Wanawake - Malkia na hata Wastaafu – Pension Account.


“Hizi ni baadhi tu ya fursa nyingi ambazo wateja na wadau wetu wanastahili ili kufikia malengo yao kwa mwaka huu 2022. Katika kipindi hiki cha kampeni tumejipanga kuhakikisha tunatoa huduma za daraja la kwanza kwa wateja wetu ili wawaeze kunufaika na fursa hizi zinazotolewa na benki yao.,” amesema Nsekela.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa amesema benki hiyo itaendelea kutekeleza ahadi yake ya kumuweka kwanza mteja na kuwakaribisha Watanzania wote, wateja binafsi, makampuni, na taasisi kuchangamkia fursa hizo kufikia malengo yao. “Benki yetu ni imara na yenye kuaminika kwa ubunifu hapa nyumbani na nje ya nchi.


Nafikiri wote tumeona tulivyopokelewa vizuri hata nchi za jirani za Burundi na Congo, na inavyoaminika na Serikali kwa kuwa na mchango mkubwa kwenye kusaidia kujenga uchumi,” alisema Tully huku akiwataka wafanyabiashara wanaofanya biashara nan chi za jirani pia kutumia fursa zinazotolewa na benki hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda aliwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuichagua benki hiyo kuwa mtoa huduma wao na kuwaahidi benki hiyo itaendelea kuwapa wanachostahili kupitia bidhaa na huduma bunifu.


--

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com