Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BODI YA FILAMU KUENDELEZA FURSA ZA KUWAINUA WASANII- WAZIRI MCHENGERWA


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa maelekezo ya kuendeleza utendaji bora kwa Taasisi za Bodi ya Filamu, BASATA na COSOTA wakati alipofanya ziara katika Taasisi hizo katika majengo ya Utumishi, Kivukoni jijini Dar es Salaam. Akifuatiwa na Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Hassan Abbas, Naibu Katibu Mkuu Mhe. Said Othman Yakubu na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas akielezea kuhusu umuhimu wa Haki za Wasanii wakati Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mohamed Mchengerwa alipozitembelea Taasisi za Bodi ya Filamu, BASATA na COSOTA zilizopo katika majengo ya Utumishi, Kivukoni jijini Dar es Salaam.


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo akielezea majukumu na utendaji wa Bodi hiyo wakati Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mohamed Mchengerwa alipozitembelea Taasisi za Bodi ya Filamu, BASATA na COSOTA zilizopo katika majengo ya Utumishi, Kivukoni jijini Dar es Salaam.

...........................................................................

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaka Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) kuendelea kuwajengea uwezo Wadau mbalimbali wa Tasnia ya Filamu kwa lengo la kuhakikisha Wadau hao wanakuwa na uwezo wa kutoa kazi zenye viwango bora.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati alipokuwa katika ziara ya kutembelea na kujifunza majukumu ya Taasisi zilizopo katika Wizara hiyo ikiwemo Bodi ya Filamu Jumatatu Januari 17, 2022 Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na Watendaji wa Bodi ya Filamu Waziri ameitaka Bodi hiyo kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo Wadau wa Filamu ili waweze kutoa Filamu za Kitanzania zenye ubora mzuri na uhalisia zitakazoweza kutangaza fursa mbalimbali ndani na nje ya nchi, hivyo kuongeza pato la Taifa.

“Tuendelee kutafuta fursa za kuwainua na kunyanyua kazi za Tasnia yetu ya Filamu ili waweze kunufaika na kufaidika na kazi zetu jambo litakalowezesha kuijenga zaidi Tasnia ya Filamu,” amesema Waziri

Aidha, Waziri amesisitiza Bodi kufuatilia utekelezaji wa uanzishaji wa Jumba Changamani ambalo litakuwa maalum katika utengenezaji wa Filamu na Michezo ya Kuigiza itakayowasaidia Wasanii kuandaa Filamu kwa urahisi na zenye viwango bora zaidi.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbas amesisitiza Taasisi za Wizara hiyo ikiwemo Bodi ya Filamu kufanya kazi kwa malengo ya kulinda na kutetea maslahi ya Wanatasnia wa Filamu ili kuwawezesha kunufaika na kazi zao za Filamu na Michezo ya kuigiza.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Dkt. Kiagho Kilonzo akiwasilisha utendaji wa Tasnia ya Filamu pamoja na majukumu ya Bodi hiyo amesema Tasnia hiyo hadi kufikia mwaka 2021 imekuwa ikichangia katika kutoa ajira takribani 30,000 zinazotokana na shughuli za utayarishaji wa Filamu.

Ameongeza kuwa Bodi hiyo tayari iko katika hatua za kuwa na Kanzidata yenye taarifa za Wanatasnia wa Filamu kwa lengo la kutambua taarifa za Wanatasnia wa Filamu kwa urahisi na usahihi zaidi.

Dkt. Kilonzo amesema Bodi hiyo tayari inaendelea kuandaa mfumo wa Kidijitali utakaosaidia kutoa huduma kwa Wanatasnia wa Filamu kwa urahisi bila kufika Ofisini hapo. Aidha mfumo huo utarahisisha utoaji wa huduma kwa Wanatasnia katika maeneo yao na kuwapunguzia gharama pamoja na kuwapa uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com