Na Dinna Maningo, Tarime.
ZIKIWA zimesalia siku saba kusherekea miaka 45 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Februari 5,mwaka1977, wilaya ya Tarime imefanikiwa kuwa na ongezeko la idadi ya wanachama wapatao 76,300 ikilinganishwa na Februari,5,2021wakati ikitimiza miaka 44 ilikuwa na wanachama 62,000.
Kuongezeka kwa idadi ya watu kujiunga na chama hicho inaelezwa kuwa inatoka na sababu mbalimbali ikiwemo ya Chama hicho kuisimamia serikali kuhakikisha inatekeleza Ilani ya CCM huku kikiwa mstari wa mbele kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua hali ambayo imesababisha chama kuwa kivutio kwa wananchi.
Wakizungumza na Malunde 1 blog Wanachama walieleza sababu ya kuongezeka kwa idadi ya wanachama ambapo Katibu wa CCM wilaya ya Tarime Valentine Maganga alisema kuwa kazi ya chama ni kuisimamia Serikali ili kuwaletea wananchi maendeleo na kutatua changamoto.
"Chama kikiisimamia serikali na ikafanya vizuri watu lazima wakipende,serikali ikifanya vibaya kinachochafuka ni chama kwakuwa ndiyo msimamizi wa serikali,mazuri yaliyofanywa na serikali yamesababisha watu kuzidi kujiunga,vijana wamejitokeza zaidi hata leo kuna watu 100 kata ya sabasaba wanataka kadi na 50 kutoka mtaa wa Buhemba", alisema Maganga.
Katibu huyo aliongeza kusema" Idadi ya watu kuongezeka ilianza 2015 na sasa 2022 idadi inazidi kuongezeka kwasababu wananchi wanaona mazuri hakuna michango mashuleni, barabara zinajengwa maeneo mengi huduma ya maji na huduma za afya,mikopo isiyo na riba na mambo mengi yamechochea CCM kupendeka".
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa viungo (CHAWATA) wilaya ya Tarime ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Jumuiya ya CCM ya Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Rosemary Masirori mkazi wa kata ya Bomani alisema kuwa vijana wengi wamepata fursa ya uongozi kwenye chama na serikalini.
"Vijana walichukuliwa kama ni watu wahuni hawawezi kuongoza na kufanya kazi,serikali ya awamu ya tano na ya sita vijana wengi wamejiunga na ccm na wengine wamevutiwa baada ya mikopo kutolewa bila riba" ,alisema Rosemary.
Acren kapwela mkazi wa kijiji cha Nyandage kata ya Nyanungu alisema kuwa mifumo mizuri ya kiuongozi ndani ya chama uwavutia wengi kwakuwa upokezana uongozi ndani ya chama jambo ambalo limewawezesha watu kupata fursa za uongozi.
"CCM ni mali ya umma ndiyo maana watu wengi wanaikubali kuna viongozi waandamizi wa serikali walihamia upinzani na kutoka CCM walipofika kule walishindwa kuendana na mifumo ya kiuongozi na uendeshaji wa vyama wakarudi CCM", alisema Kapwela.
Samwel Paschal alisema kuwa utawala wa uongozi wa Hayati John Magufuli ulichochea wengi kujiunga na CCM kwakuwa aliwajali wanyonge na wamachinga na kutatua kero zao papohapo huku miradi mikubwa ya maendeleo ikitekelezwa nakwamba aliwaonyesha wananchi namna mzuri ya kutumia rasilimali za taifa na kuwafundisha watanzania kujitegemea.
Sherehe hizo za kumbukizi ya kuzaliwa kwa chama hicho kitaifa zitafanyika februari,5,2022 katika mkoa wa Mara huku mgeni rasmi akiwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu.