Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZAZI WALALAMIKA KUTOZWA 5,000 WANAPOANDIKISHA WANAFUNZI DARASA LA KWANZA


 Muonekano wa shule ya Msingi Buguti Nkongo Wandiba
Na Dinna Maningo, Tarime


BAADHI ya Wazazi kata ya Turwa wilaya ya Tarime wamemlalamikia mkuu wa shule ya Msingi Buguti Nkongo Wandiba kwa kuwatoza Wazazi fedha sh.5,000/= wanapofika kuwaandikisha watoto darasa la kwanza nakwamba kwa wale wazazi wasiokuwa na fedha utishiwa watoto wao kutosajiliwa hadi pale watakapolipa fedha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Chacha Marwa mkazi wa mtaa wa Kebikiri alisema kuwa Mkuu huyo wa shule amekuwa akiomba fedha za uandikishaji wa watoto jambo ambalo limempa utata kwa kile alichoeleza kuwa Rais Samia Suluhu alitoa fedha zitokanazo na Uviko kujenga madarasa katika shule zenye upungufu wa madarasa lakini wanatozwa fedha.


"Rais wetu mama yetu mpendwa mwenye huruma na wananchi aliona atuondolee adha ya michango akatoa fedha kwenye halmashauri mbalimbali nchini ikiwemo halmashsuri yetu lakini tunashangaa tunaombwa fedha inamana hii shule kama ilikuwa na upungufu wa madarasa kwanini yenyewe haikutengewa fedha hadi tunaombwa fedha ya majengo?

Aliongeza" watoto tunaandikisha ofisi ya mwalimu mkuu ukifika unamkuta yeye na mwalimu mwingine wa kike ,utaombwa cheti cha kuzaliwa au barua ya Mwenyekiti wa mtaa ya utambulisho wa mtoto kisha anaandikwa alafu unaombwa 5,000 ukihoji ni ya nini unaambiwa sh. 3,000 ni mchango wa ujenzi,1,000 pesa ya mlinzi na 1,000 pesa kwa ajili ya kuandaliwa kadi ya matokeo mwanafunzi anapofanya mtihani",alisema Marwa.


Bhoke Ryoba mkazi wa mtaa wa Kokehogoma aliongeza" kama hauna pesa mkuu wa shule anamwambia yule mwalimu wa kike futa jina la huyo mtoto siku atakapoleta pesa ndipo atasajiliwa inabidi uende utafute pesa upeleke mwanao aandikishwe shule",alisema.


Rebeka Yusuphu mkazi wa mtaa wa Kebikiri alisema kuwa ni desturi ya mkuu huyo kuchangisha wazazi pesa kila mwaka watoto wanapoandikishwa darasa la kwanza licha yakwamba michango ya ujenzi wa shule uchangishwa kwenye mitaa yao kupitia viongozi wa serikali za mitaa.

"Mwaka jana niliandikisha mtoto nikalipa sh.8,000 tuliombwa na mkuu wa shule akasema ni pesa ya majengo ,mlinzi,kadi na pesa kwa ajili ya fotokopi za mitihani,hiyo michango tunaombwa bila sisi wananchi au wazazi kushirikishwa ili tujadili.

"Serikali ilishakataa walimu wasichangishe na kupokea fedha lakini huyu mkuu wa shule ndiyo amekuwa akipokea fedha wanafunzi wanapojiunga shule na michango mingine", alisema Rebeka.

Baadhi ya Wenyeviti wa mtaa akiwemo Mwenyekiti wa mtaa wa Kokehogoma Musa Nehemia alisema kuwa hakuna kikao kilichoketi kujadili na kupitisha michango ya watoto wanaosajiliwa darasa la kwanza nakwamba wazazi hawatakiwi kutoa fedha kwakuwa hakuna taarifa yoyote iliyofika kwenye mitaa au kujadiliwa kwenye vikao vya ngazi ya kata vikionyesha uwepo wa upungufu wa majengo yanayohitaji kuchangisha wazazi fedha.

"Na mimi nimepata taarifa kwa baadhi ya wazazi kudai kuchangishwa fedha wanapoenda kuandikisha watoto,mimi ninachofahamu kukiwa na uhitaji wa maendeleo ya shule huwa tunakaa vikao vya WDC tunawaambia wazazi wa wanafunzi tunajadili tunapanga au tunawapelekea wananchi nao wanajadili na kupitisha michango kila mtaa unapanga.

" Kisha wananchi wanachanga fedha majengo yanajengwa na kamati za shule zinasimamia ujenzi,mi nimewazuia wananchi wasichange na ntafatilia kwa mwalimu kujua kwanini anatoza wanafunzi michango",alisema Nehemia.


Mkuu wa shule ya Msingi Buguti Nkongo Wandiba alikiri wazazi kutozwa sh.5,000 nakusema kuwa michango hiyo ilipitishwa kwenye kikao cha wazazi mwezi Februari,2021,licha ya kauli hiyo kupingwa na wazazi kuwa hakuna kikao kilichoketi kujadili michango huku wakiongeza kuwa vikao vya 2021 haviwezi kutumika kwakuwa sasa ni 2022 vikao vinatakiwa kuitishwa upya na kujadili michango.

"3,000 ni pesa ya ujenzi wa majengo ilipitishwa na wazazi Aprili 2021, 1,000 ni pesa ya mlinzi hili lilijadiliwa na likapelekwa hadi ofisi ya Dc na likapitishwa,1,000 ni pesa ya kadi kwa ajili ya kujaziwa matokeo ila yenyewe siyo lazima utoe pesa unaweza ukanunua mitaani ukaleta", alisema.

Akizungumzia kuhusu michango hiyo kwanini haipelekwi kwa viongozi wa serikali za mtaa badala yake kuwasilishwa moja kwa moja shuleni alisema"hii michango haitangazwi kwenye mikutano ya wananchi unaleta pesa moja kwa moja shuleni kwakuwa ilishapitishwa na wazazi,ukisema umsajili mtoto ndiyo mzazi alete pesa hawaleti"alisema Wandiba.

Mratibu Elimu kata ya Turwa Imani Buchafya alisema kuwa Desemba 6,2021 kiliketi kikao cha wakuu wote wa shule kwenye kata hiyo ambapo wakuu wa shule walitakiwa kutowachangisha wazazi michango wala kuwabughudhi watoto kuhusu michango nakuahidi kufatilia kwa kile alichoeleza kuwa hajapokea taarifa ya wazazi kuchangishwa fedha.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Turwa Marwa Timoro (Sheby) alisema kuwa hata yeye amepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi wakidai kuombwa sh.5,000 na amepiga marufuku michango kwa wanafunzi wanaoandikishwa nakwamba iwapo kuna uhitaji wa michango taratibu zifuatwe ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wazazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com