Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GEKUL AFUNGUA SHEREHE ZA SIKU YA UTAMADUNI KATIKA CHUO CHA NDC-TZ


******************

Na John Mapepele

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amefungua sherehe za siku ya utamaduni katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC-TZ) leo Januari 28, 2022 jijini Dar es Salaam.

Akifungua sherehe hizo Mhe.Gekul amesema tukio hilo ni mahususi ambalo limelenga kuheshimu utamaduni wetu na tamaduni zingine nje ya mipaka yetu na bara zima kwa ujumla wake.

“Niwasihi wageni wote waalikwa, Wanachama pamoja na nchi marafiki za Bangladeshi, Botswana, Misri, Malawi, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Burundi, Kenya, Nigeria, na Rwanda nyote mjaribu kadri muwezavyo kupenda na kujivunia utamaduni wenu. Naamini, kupitia utamaduni watu wanaweza kuleta mabadiliko kwa kufanya kazi na kushirikiana na watu mbalimbali” amefafanua

Amesema tukio la mwaka huu ni la kipekee sana na muhimu zaidi, kwa kuwa linakumbusha kupenda na kuthamini tamaduni zetu. “Hasa mimi ninayetoka katika Wizara yenye dhamana ya utamaduni nimefarijika sana, kwani kwa hakika tukio hili ni utekelezaji wa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ambayo inawataka wadau wote kushiriki katika kuendeleza Utamaduni” ameongeza Mhe. Gekul

Amesema Afrika inaaminika kuwa na utajiri mkubwa wa tamaduni na imebarikiwa kuwa na maumbo ya kipekee kama milima na mabonde, wanyama pori, vyanzo mbalimbali vya maji na pia ukarimu wa watu katika bara hili, hivyo kuna kila sababu ya kuuenzi.

Aidha ameongeza kuwa Tanzania ina zaidi ya makabila 120 na lugha zaidi ya 120 ambapo amesema kinachovutia zaidi, makabila haya yote yana tamaduni zao na kuunganishwa na lugha moja ya Kiswahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com