VIGOGO WALIOTEMWA BARAZA LA MAWAZIRI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi, Januari 8, 2022 amefanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambapo ameingiza mawaziri wapya na manaibu waziri huku akiwaacha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji, Geofrey Mwambe.

Kwa upande wa Manaibu Waziri walioachwa ni Mwita Waitara ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, aliyekuwa Naibu wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chilo.


Tisa wabadilishwa wizara

Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaongozwa na Waziri mpya Jenista Mhagama ambaye amehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Ajira Vijana na watu wenye Ulemavu.

Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa atakuwa Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo kuchukua nafasi ya Inocent Bashungwa.

Innocent Bashungwa, anakuwa Waziri mpya wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Ummy Mwalimu, aliyehamishiwa Wizara ya Afya.

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Dorothy Gwajima sasa nataongoza wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watu wenye mahitaji maalum.

Aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchui Kenya, Pindi Chana sasa ameteuliwa kuongoza Wizara ya Sera na Bunge katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri Mwingine Katika Ofisi ya Waziri Mkuu ni Profesa Joyce Ndalichako atakayeshugulika na Kazi na Ajira ambaye amehamishwa kutoka Wizara ya Elimu, Syansi na Teknolojia.


Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi sasa itaongozwa na Masauni Yusuph Masauni aliyepandishwa wadhifa kutoka Naibu waziri na anachukua nafasi ya Simbachawene, aliyehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.

Simbachawene anachukua nafasi ya Prof. Palamagamba Kabudi ambaye ameachwa nje ya baraza.

Pia Aliyekuwa Naibu waziri wa Kilimo, Husseon Bashe sasa anakuwa waziri kamili akichukua nafasi ya Profesa Adolf Mkenda aliyehamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Naibu waziri mwingine aliyepandishwa cheo ni Anjelina Mabula atakayeongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi kuchukua nafasi ya William Lukuvi, mwanasiasa mkongwe aliyedumu katika nafasi za juu serikali kwa muda mrefu na pia ni mbunge wa Ismani mkoani Iringa kwa zaidi ya miaka 25.

Dkt. Ashatu Kijaji sasa ni Waziri mpya wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara akihamishwa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na anachukua nafasi ya Prof. Kitila Mkubo na Geoffrey Mwambe(Uwekezaji) ambao wameachwa nje baraza jipya.

Nape Nnauye ndiye Waziri mpya wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alikotoka Dkt Kijaji. Nape aliwahi kuongoza Wizara ya Habari na kuondolewa mwaka 2017 na Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Mawaziri waliobakia katika nafasi zao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberatha Mulamula; Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba; Waziri wa Nishati, January Mkamba; Waziri wa Madini, Doto Biteko; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro; Waziri wa Maji, Jumaa Aweso; Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa; Waziri wa Ulinzi, Stegomena Tax; na Waziri Ofisi ya Rais - Kazi Maalum, George Mkuchika.







 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم