Hatua ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpitisha Dkt. Tulia Ackson kuwa mgombea wake wa nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania kumefungua ukurasa mwingine katika maisha ya kisiasa yasiyo ya kawaida ya mbunge huyu wa Mbeya Mjini katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Kwa hatua hii ya Kamati Kuu ya CCM, njia sasa ni nyeupe kwake kuwa Spika wa saba wa Bunge la Tanzania kwa vile mhimili huo sasa una wingi mkubwa wa wabunge kutoka chama tawala na hakuna uwezekano wa wabunge wa chama hicho kuacha kumchagua mgombea ambaye amepitishwa na chama chao.
Katika mkutano wa muda mfupi na waandishi wa habari uliofanyika Alhamisi Januari 20 2022, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, alimtangaza Tulia kwamba ndiye chama kitampeleka kupigiwa kura na wabunge Februari mosi kwenye uchaguzi wa Spika.
Tulia Ackson ni nani hasa na kwanini safari yake siyo ya kawaida?
Katika historia ya takribani nusu karne ya Bunge la Tanzania, wana CCM waliokuwa wakipewa nafasi ya kuwania Uspika walikuwa na sifa tofauti lakini moja haikuwahi kubadilika nayo ni uzoefu wa ubunge na katika siasa za kitaifa.
Spika wa kwanza, Adam Sapi, alikuwa ndiye mbunge wa muda mrefu zaidi wakati akipewa madaraka yake hayo, alimyemfuata - Pius Msekwa, alikuwa na uzoefu wa ubunge na kitaasisi wa takribani miaka 30 na hivyo hivyo kwa Samuel Sitta na Anne Makinda. Mtangulizi wa Spika anayefuata, Job Ndugai, tayari alikuwa mbunge kwa miaka 15 wakati anapitishwa na CCM kuwania uspika kwa mara ya kwanza mwaka 2015.
Hadi kufikia mwaka 2015, Tulia hakuwa akifahamika sana nje ya duru za kisheria na kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikosoma shahada mbili za sheria na baadaye kuwa mhadhiri wa Sheria katika Kitivo cha Sheria cha chuo hicho kikongwe na maarufu zaidi nchini Tanzania.
Mara ya kwanza kuanza kujulikana nje ya duru za kisheria ilikuwa ni Februari mwaka 2014, wakati Rais Jakaya Kikwete alipomteua kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba akiwakilisha Jumuiya na Taasisi za Elimu ya Juu. Ni Kikwete huyo huyo aliyemteua Tulia kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipofika Septemba mwaka 2015.
Huo ndiyo uteuzi ambao hasa ulimtambulisha Tulia kwa jamii ya Watanzania. Novemba mwaka 2015, yaani miezi miwili tu katika nafasi ya Naibu Mwansheria Mkuu wa Serikali, Rais John Magufuli - katika mojawapo ya uteuzi wake wa mwanzoni wa wabunge katika nafasi 10 anazoruhusiwa kikatiba, alimteua Tulia kuwa mbunge na kumuondoa katika nafasi yake aliyoteuliwa na Kikwete.
Kwa wafuatiliaji wa siasa za kibunge, huo ulikuwa ni ushahidi kwamba kwa vile Ndugai hakuwa sehemu ya watu wa karibu na Magufuli, mbunge huyo za zamani wa Jimbo la Chato, alitaka kuwa na 'mtu wake' katika nafasi hiyo ya pili kwa ukubwa ndani ya mhimili wa Bunge. Kwa sababu hiyo, walau katika siku zake za mwanzoni za unaibu Spika, Tulia alikuwa akionekana kama tu 'mtu wa Magufuli' - kwa sababu ya namna alivyoteuliwa kuwa mbunge na jinsi alivyopata cheo hicho bungeni.
Kawaida isiyo ya kawaida
Katika utumishi wake wa unaibu Spika, Tulia alipata pia uzoefu mwingine ambao pengine hakuna mtangulizi wake mwingine alipata kuwa nao. Kuna jambo moja lisilo la kawaida lilitokea lililompa Tulia jambo ambalo manaibu Spika waliomtangulia hawakulipata.
Jambo hilo lilikuwa ni kuugua kwa Ndugai. Miezi michache tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Ndugai alipata changamoto za kiafya zilizosababisha aende kutibiwa nje ya nchi alikokaa kwa takribani miezi sita. Changamoto hiyo ilisababisha Tulia aanze kufanya kazi ambazo kwa kawaida Spika huwa hamwachii naibu wake azifanye.
Kwa kifupi, katika wakati wa ugonjwa wa Ndugai, Tulia alikuwa kama Spika kamili asiye na cheo tu cha kuthibitishwa. Kuna historia ya migongano ya kikazi kati ya Spika na Naibu katika Bunge la Tanzania lakini Tulia - katika bahati ya peke yake, hakuwa nayo katika miezi yake ya kwanza kwenye cheo hicho kwa sababu bosi wake hakuwepo.
Ni katika mazingira hayo ambapo jambo lingine lilitokea kwa Tulia. Katika taratibu za CCM, Spika wa Bunge ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Kwa kawaida, naibu Spika huwa haingii katika Kamati Kuu - lakini Mwenyekiti wa CCM, Magufuli alimruhusu Tulia kuingia katika vikao hivyo na kuondoa ule utamaduni kwamba ni cheo ndiyo kinaingia kwenye vikao na si mtu.
Kwa sababu hiyo, pamoja na kwamba kulikuwa na wagombea wengine wa uspika kupitia CCM, ambao pengine walikuwa na uzoefu kisiasa na kibunge kumzidi Tulia, kwa maana ya uzoefu hasa wa kuwa Spika - ni mwanasheria huyo mwenye umri wa miaka 45 ndiye pekee ambaye angeweza kujidai kwamba amewahi kuwa 'Spika'.
Kwanini CCM imempitisha Tulia?
Sababu ya kwanza iliyo wazi ni kwamba katika utaratibu wa miaka ya karibuni, Naibu Spika wa Bunge ana nafasi kubwa ya kuwa Spika kwenye uchaguzi unaofuata. Msekwa alikuwa naibu wa Mkwawa, Makinda alikuwa naibu wa Sitta na Ndugai alikuwa naibu wa Makinda. Kimsingi, katika historia ya Bunge la vyama vingi hapa Tanzania, ni Sitta pekee ndiye aliyekuwa Spika pasipo kuwahi kuwa naibu awali.
Uspika wa Tulia ni mwendelezo wa hali iliyopo. Kupitishwa kwa Tulia ni ishara kwamba chama kimeamua kuendelea na waliopo - jambo ambalo kimsingi ndiyo mojawapo ya alama kubwa za utawala wa Rais Samia Saluhu Hassan.
Lakini Tulia ana sifa nyingine nne za ziada ambazo ni muhimu kuwekwa kwenye mjadala. Moja ni jinsi yake - kwamba Tanzania sasa; kwa mara ya kwanza, inakwenda kuwa na viongozi wawili wa mihimili ya dola yenye jinsi ya kike na sitashangaa kama nchi inaweza kushuhudia kuja kuwa na Jaji Mkuu mwanamke kwa mara ya kwanza na kukamilisha "Utatu" wa kwanza wa wanawake kuongoza mihimili yote ya dola. Wanaume wameongoza mara nyingi mihimili yote hiyo kwa wakati mmoja - kuondoa wakati wa Makinda - Spika wa kwanza mwanamke, na pengine huu ni wakati wa kubadili mazoea.
Jambo la pili ni tabia ya Tulia. Kwa marafiki zake na watu wanaofahamu tabia zake, yeye si mtu wa kugombana na mamlaka. Mara zote amekuwa mtiifu - iwe kazini au kwenye shughuli nyingine na hiyo ni tabia iliyomfanya awe kipenzi cha mmoja wa walimu wake na walezi wake wa kisiasa, Dkt. Asha Rose Migiro Waziri wa zamani wa Mambo ya nje wa Tanzania pia Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa; enzi wote wakiwa UDSM.
Katika mazingira ya sasa ya Urais wa Samia, Spika mwenye tabia za utata na kuibua maneno asingeweza kuendana na serikali. Na bahati - katika kuonesha kukua kisiasa kwa Tulia, alitumia nafasi ya kuzungumza mbele ya Samia wiki iliyopita wakat iwa kuwaapisha mawaziri wapya, kumthibitishia Rais kwamba Bunge litakuwa rafiki kwa serikali na kwamba "Rais yuko juu ya mihimili mingine ya dola". Pengine ile ndiyo siku ambayo nafasi yake kwenye uspika ilithibitishwa kwenye macho ya dola.
Jambo la tatu ni mahali anakotoka kisiasa. 'Mpakwa mafuta' huyu kwa tiketi ya CCM ni mwenyeji wa mkoa wa Mbeya ambao katika miaka ya karibuni umekuwa sehemu ya vitovu vya siasa za upinzani. Kustaafu siasa kwa Profesa Mark Mwandosya kuliuondolea mkoa huo na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwanasiasa mwenye ushawishi wa ngazi za juu. Uteuzi wa Tulia - na iwapo atafanikiwa kuwa Spika kama inavyotarajiwa, unairudisha Mbeya na mikoa hiyo katika siasa za juu. Kwa maana nyingine, Tulia sasa anakwenda kuwa "Binti Mfalme" wa CCM katika mikoa hiyo muhimu kisiasa.
Nne, kwa umri wa wake wa miaka 45, Tulia ni miongoni mwa kundi la wanasiasa vijana na mara nyingi huwa hafichi kuonyesha hilo. Wapenzi wa mchezo wa soka, kwa mfano, wanamfahamu kwamba ni shabiki wa timu ya mpira ya Simba na amekuwa akiposti video akiwa anacheza miziki ya wanamuziki mashuhuri wa muziki wa kizazi kipya kama vile Harmonize na Diamond. Uamuzi wa kumpa Tulia nafasi ni uamuzi wa kuonyesha imani kwa vijana. Akishinda, atakuwa ndiye Spika kijana zaidi katika historia ya Bunge la vyama vingi nchini Tanzania.
Historia ya Tulia kwa ufupi
Tulia alizaliwa katika Kijiji cha Bulyaga, wilayani Tukuyu mkoani Mbeya mnamo Novemba 23 mwaka 1976. Ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika sheria kutoka katika Chuo Kikuu mashuhuri cha Cape Town, Afrika Kusini.
Alianza elimu yake ya Msingi katika Shule ya Mabonde na kupata elimu ya awali ya sekondari kwenye shule ya Loleza iliyopo Mbeya. Kwa masomo ya sekondari ya juu, Tulia alisoma katika Shule ya Zanaki jijini Dar es Salaam.
Aliajiriwa na UDSM mwaka 2001 kama mhadhiri msaidizi mara baada ya kumaliza masomo yake ya shahada ya kwanza na ya pili ambapo alikuwa mmoja wa wanafunzi bora katika kitivo cha sheria.
Tulia ameolewa, mumewe anaitwa James Mwainyekule.
CHANZO - BBC SWAHILI
Social Plugin