Polisi nchini Liberia wamemkamata na kumfungulia mashtaka mwanaume wa Sierra Leone mwenye umri wa miaka 29 kwa madai ya kujaribu kumuuza mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 10.
Inaonekana ilikuwa ni jitihada kubwa ya kutafuta pesa za kununua pikipiki mpya baada ya aliyokuwa nayo kuibwa .
Baada ya kukamatwa, mwanamume huyo aliwaambia maafisa wa uchunguzi katika mji mkuu, Monrovia, kwamba alihitaji karibu $1,000 (£750) kwani pikipiki hiyo, ambayo ilikuwa ya rafiki yake, ilikuwa imeibiwa nyumbani kwake.
Aliambiwa njia pekee ya kupata pesa nyingi hivi haraka ni kwenda nchi jirani ya Liberia kujaribu kutafuta mnunuzi wa mtoto wake.
nyumbani kwao watu walikuwa wamemwambia itakuwa rahisi kufanya mauzo ya aina hiyo katika eneo la mpakani
Ilipangwa kupitia mtu wa kati mnamo Desemba. Wakati wa mazungumzo mvulana huyo alijulikana kama kuku na sio binadamu ili kuepusha kugunduliwa.
Hata hivyo polisi walipokea taarifa, na babake akakamatwa kwani mnunuzi aliripotiwa kuwa njiani kumchukua mvulana huyo kutoka mji nje ya Monrovia.
Kulingana na chapisho la mtandaoni la Liberia Global News Network, mtoto huyo kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa wizara ya jinsia.
Ulanguzi wa binadamu ni suala kubwa katika Afrika Magharibi.
Watoto wanaouzwa katika utumwa wa kisasa hawaruhusiwi kuwasiliana na familia zao na mara nyingi wanalazimishwa kufanya kazi kama watumishi wa nyumbani au vibarua.
CHANZO- BBC Swahili
Social Plugin