Afisa Msimamizi Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Paul Ramadhan (kulia) akimuelimisha mfanyabiashara wa duka la jumla sokoni Kariakoo jijini Dar es Salaam leo 06/01/2022 kuhusu matumizi ya mashine za EFD na faida zake wakati wa kampeni ya matumizi ya mashine za EFD sokoni hapo.
Afisa Msimamizi Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Benny Macoro (kulia) akichukua taarifa za EFD kutoka kwa mfanyabiashara wa duka la jumla sokoni Kariakoo jijini Dar es Salaam leo 06/01/2022 wakati wa kampeni ya matumizi ya mashine za EFD sokoni hapo.
Afisa Msimamizi Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Samwel Kimaro (kulia) akimuelimisha mfanyabiashara wa duka la wino wa printa leo 06/01/2022 sokoni Kariakoo jijini Dar es Salaam kuhusu utunzaji wa kumbukumbu za biashara na utoaji sahihi wa risiti za EFD wakati wa kampeni ya matumizi ya mashine za EFD sokoni hapo.
*****************************
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea na kampeni ya matumizi ya mashine za kielektroniki za EFD inayojumuisha kukusanya taarifa za namba za utambulisho wa mlipakodi yaani TIN, namba za utambulisho wa mashine za EFD za eneo la biashara, namba za simu za wamiliki wa biashara pamoja na aina za biashara katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kampeni hiyo endelevu, Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka TRA Mkoa wa Kodi wa Ilala jijini Dar es Salaam, Bw. Paul Ramadhani amesema kuwa, lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanajenga utamaduni wa kutoa risiti halali za EFD kulingana na mauzo au huduma wanazotoa na wanunuzi wanadai risiti za EFD pindi wanapofanya manunuzi yao.
“Lengo hasa la TRA kufanya kampeni hii endelevu ni kuhakikisha kuwa, wafanyabishara wanakuwa na utaratibu wa kutoa risiti kwa mujibu wa sheria kila wanapofanya mauzo ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wanunuzi kudai risiti kila wanaponunua bidhaa”, alisema Bw. Ramadhan.
Kwa upande wa baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kufanya kampeni hiyo ambapo wamesema kuwa, zoezi hilo linawasaidia kuwakumbusha wajibu wao wa kutoa risiti ambazo zinasaidia katika kukadiria kodi na kutunza kumbukumbu za mauzo yao halisi.
“Zoezi hili ni zuri maana katika ubinadamu kuna kujisahau lakini maofisa wa TRA wanapofanya zoezi hili mara kwa mara, linatusaidia kuwa makini kutoa risiti kila tunapouza bidhaa zetu”, alisema Bi. Glory Msuja ambaye ni mfanyabiashara wa Kariakoo.
Mfanyabiashara mwingine aliyeipongeza TRA kwa kufanya kampeni ya matumizi ya EFD ni Bw. Abdul-Rashid Mohamed ambaye pamoja na pongezi hizo, ameiomba TRA iendelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kudai risiti na kuwa waelewa pale wanapoambiwa bei stahiki badala ya kung’ang’ania kupunguziwa bei.
Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na kampeni ya matumizi ya mashine za EFD katika mitaa yote ya Kariakoo jijini Dar es Salaam na kwa sasa kampeni hiyo inafanyika katika mitaa ya Lindi, Congo, Msimbazi na Uhuru.