Watu wawili wamepoteza maisha na wengine nane (8) kujeruhiwa, hii leo Januari 28, 2022, katika ajali iliyohususha lori na watembea kwa miguu maeneo ya Kimara Suka Jijini Dar es salaam, baada ya dereva wa lori hilo kupita kwenye kivuko cha watembea kwa miguu bila kuchukua tahadhari.
Taarifa ya ajali hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, na kusema kuwa ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa dereva wa lori ambaye amekimbia baada ya kusababisha ajali hiyo.
Aidha Kamanda Muliro, amesema kuwa majeruhi wote katika ajali hiyo walikimbizwa katika hospitali ya Bochi.
Mashuhuda wa ajali hiyo wameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo gari hilo lilionekana kupoteza mwelekeo baada ya kufeli breki na kuwapitia watembea kwa miguu waliokuwa eneo hilo hivyo kusababisha vifo vyao na majeruhi.
“Mimi nimesimama pembeni naona gari linanifuata na lilikuwa katika spidi kubwa sana niliruka mtaroni ndicho kilichonisaidia bila hivyo sijui,” amesema John Kelvin aliyekuwa amepaki boda boda yake pembeni.
“Rafiki yangu mshtuko alikimbia mbio limemkuta huko huko nikamuona anaingia chini ya lori ndio wamemtoa ameshakufa jamani,” amesema.
Mmoja wa ndugu wa majeruhi ambaye hakuta jina lake kuandikwa amesema amefuatwa nyumbani na boda boda akaambiwa mke wake Aisha amekatika sikio.
“Nilitoka nyumbani haraka sana, nilikuwa mke wangu amewekwa kwenye Kirikuu nikamtoa nimeleta mwenyewe hapa Bochi nikasaidia na wengine wawili.
“Ajali ni mbaya jamani maana imewafuata watu pembeni mimi mke wangu alikuwa anaenda kazini jamani hali yake sio nzuri,” amesema.
Social Plugin