Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFUGAJI WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUWAKUMBUKA NA KUWAJENGEA MADARASA

Chifu mkuu wa mikoa saba wa Kabila hilo la Wamasai Chifu Kashu Moreto

Na Jackline Lolah Minja -Morogoro

Wafugaji jamii ya Kimasai Kitongoji cha Manyara kijiji cha Twatwatwa wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wamempongeza Rais Samia kwa kuwakumbuka jamii hiyo ambayo ilisahaulika katika sekta ya elimu kwa kuwajengea madarasa matatu kupitia fedha za  Taifa za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO - 19.

Akizungumza katika hafla fupi ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa Ujenzi wa madarasa hayo, Chifu mkuu wa mikoa saba wa Kabila hilo la Wamasai Chifu Kashu Moreto amesema wanamshukuru serikali kwa kuwakumbuka jamii yao katika jitihada ya kuinua taaluma.

Chifu Moreto anasema awali jamii ya kifugaji hasa Wamasai ilisahaulika katika sekta ya elimu lakini serikali ya awamu ya sita Chini ya Rais Jemedari Samia Suluhu Hassan amefanikisha Ujenzi wa madarasa hayo Jambo ambalo limewapa hamasa wafugaji kusomesha watoto wao

"Wafugaji tulikuwa tunaonekana kama hatuwezi kusoma kutokana na wengine kujikita katika mifugo lakini ujenzi wa vyumba hivi unahamasisha wazazi jamii ya kifugaji kusomesha watoto", amesema Kashu Moreto Chifu Mkuu Wamasai

Ameongeza kuwa baada ya kupata madarasa hayo zawadi pekee ambayo wataitoa kwa Rais Samia ni kuwapeleka watoto wao shule wakapate elimu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na kwamba hakuna mtoto wa kike atakayekosa masomo kwa sababu yeyote ile

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilosa Alhj Majd Mwanga amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wa kike badala yake wawapeleke shule kwani watoto wa kike wana vipaji vya kusoma.

DC Mwanga anasema ni marufuku mzazi kumpa mifugo mtoto mdogo kwenda kuchunga badala ya kumpeleka shule na atakaebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

"Nimeshaelekeza wazazi wote kuhakikisha wameshasaini mikataba na kuhakikisha wanawapeleka watoto shule na wanawasimamia kwa miaka yote minne, kwa hiyo ikifika kidato cha pili akaenda kuchunga ng'ombe au akaenda kuolewa na tukabaini kidato cha nne hajafanya mtihani huyo mzazi tutamuwajibisha”, amesema.

Naye Mbunge wa Kilosa Profesa Palamagamba Kabudi ameahidi kushirikiana na jamii hiyo katika kuinua elimu katika Ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

Profesa Kabudi ameongeza kwa kusema kuwa licha ya Rais Samia kuwajengea madarasa matatu bado serikali itaendelea kuwa pamoja na kuahidi kusaidia Ujenzi wa nyumba za walimu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com