MASOLWA : UKUAJI WA UCHUMI ULIONGEZEKA KIPINDI CHA JULAI HADI SEPTEMBA 2021


Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za uchumi,Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS),Daniel Masolwa akieleza namna ukuaji wa uchumi katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021,uliovyongezeka hadi kufikia kiwango cha asilimia 5.2 .

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog-DODOMA.

KAIMU Mkurugenzi wa Takwimu za uchumi,Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS),Daniel Masolwa amesema ukuaji wa uchumi katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021,uliongezeka hadi kiwango cha asilimia 5.2 kutoka asilimia 4.4 kipindi kama hicho mwaka 2020.

Masolwa ameeleza hayo leo jijini Dodoma wakati   akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukuaji wa uchumi kipindi Julai hadi Septemba mwaka 2021 huku akieleza kuwa pato la taifa kwa bei za miaka husika liliongezeka hadi shilingi trilioni 37.0 kutoka shilingi trilioni 34.5 kipindi kama hicho mwaka 2020.

Alisema pato halisi la taifa liliongezeka hadi shilingi trilioni 32.0 mwaka 2021 kutoka shilingi trilioni 30.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

"Katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021,pamoja na changamoto za Uvico-19 uchumi umeendelea kuimarika ambapo shughuli za huduma za malazi na chakula iliongezeka Kwa kiwango cha juu zaidi cha asilimia 14.3 ikilinganishwa na kiwango hasi cha asilimia 25.1 kipindi kama hicho mwaka 2020,"alisema.

Pamoja na hayo alieleza kuwa ukuaji wa uchumi huo ulichangiwa na kuongezeka kwa watalii laki  2.43 walioingia nchini kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2021 ikilinganishwa na watalii 72,147 kipindi kama hicho mwaka 2020,"alisema.

Akizungumzia ukuaji wa shughuli za kiuchumi Masolwa alisema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021,shughuli ya huduma za malazi na chakula iliongoza kwa kiwango cha juu zaidi caha ukuaji wa asilimia 14.3 ikifuatiwa na uchimbaji wa madini na mawe kwa asilimia 12.2 na huduma zingine za jamii zikijumuisha Sanaa na Burudani na shughuli za kaya katika kuajiri asilimia 12.1,umeme asilimia 10.0 na Habari na Mawasiliano kwa asilimia 9.3.

Kwenye mchango wa shughuli kuu za kiuchumi alisema mchango wa shughuli za kiuchumi umeainishwa kwa kuzingatia mchanganuo wa shughuli kuu za kiuchumi huku shughuli za huduma zikiwa na mchango mkubwa zaidi ya asilimia 42.1 ya pato la Taifa zikifuatiwa na shughuli za msingi kwa asilimia 30.1 na shughuli za kati kwa asilimia 27.8.

Alisema mchango katika ukuaji wa uchumi katika robo ya tatu ya mwaka 2021 ulikuwa  asilimia 5.2 ambapo ulichangiwa na shughuli zote za uchumi huku shughuli zilizokuwa na mchango mkubwa katika ukuaji zilikuwa ni ujenzi asilimia 18.1,kilimo asilimia 15.1,uchimbaji wa madini na mawe kwa asilimia 11.4,uzalishaji viwanda asilimia 8.6,utawala na ulinzi asilimia 5.8 na biashara na matengenezo kwa asilimia 4.0.

Hata hivyo alizungumzia Makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Dunia kwa mwaka 2021 ambapo alisema kwa mujibu wa makadirio ya shirika la fedha Duniani (IMF) ya mwezi Oktoba 2021 uchumi wa dunia kwa mwaka 2021 huku makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Dunia kwa mwaka 2022 yameendelea kubaki katika kiwango cha asilimia 4.9 zilizokuwa zimekadiriwa awali.

Pia alizungumzia ukuaji wa uchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kipindi cha Julai hadi Septemba alisema uchumi wa nchi katika Jumuiya umeendelea kuimarika kutoka kiwango hasi cha ukuaji hadi kiwango chanya.

"Hadi leo(jana) tarehe 4 Januari 2022 nchi tatu kati ya sita zimekamilisha kutayarisha na kusambaza taarifa ya pato la Taifa na taarifa za pato la Taifa robo ya tatu ya mwaka 2021 zinaonyesha kuwa uchumi wa Rwanda uliongezeka kwa asilimia 10.1 ikilinganishwa na kiwango hasi caha asilimia 3.6 kipindi  kama hicho kwa mwaka 2020,Uganda uchumi uliongezeka kwa asilimia 3.8 ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 0.8 kipindi kama hicho mwaka 2020,"alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post