MTOTO anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 13 hadi 16 amefariki dunia baada ya kuchomwa kisu shingoni wakati akigombana na mwenzake.
Ugomvi huo umehusisha watoto wa mtaani ambao wanadaiwa kuwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya gundi katika eneo la Nyerere Square jijini Dodoma.
Mfanyabiashara wa matunda katika eneo hilo, Ibrahim Juma amesema baada ya tukio hilo waliawauliza baadhi ya watoto katika eneo hilo ambapo walidai kuwa marehemu alikuwa na gundi huku mtuhumiwa akimlazimisha kumpa.
Amesema baada ya marehemu kuona anafanyiwa uonevu alichukua jiwe na kumpiga mtuhumiwa kichwani na baadaye mtuhumiwa alichomoa kisu na kumchoma mwenzake nyuma ya shingo.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma Onesmo Lyanga amethibitisha kutokea tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa. Kamanda Lyanga amesema tukio hilo limetokea jana Jumanne na Jeshi la Polisi linafanya kazi ya kuwakamata watoto hao na kuwafikisha kwenye madawati ya ustawi wa jamii.
“Sisi kama polisi tunawakamata hao waraibu na kwasababu sio kosa la jinai huwezi kusema unamshikilia kisheria kwa hiyo tunawapeleka kwa ustawi wa jamii lakini baada ya muda tunashangaa wanarudi kufanya vitendo kama hivyo, hatujajua huko kuna shida gani” amesema
Social Plugin