Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGEJA AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UTEUZI WA MAWAZIRI, AWATAKA WAHAFIDHINA WAACHE KUCHAFUA VIONGOZI


Khamis Mgeja
*
MUDA mfupi mara baada ya kuapishwa kwa mawaziri wapya ambao wameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation ya mjini Kahama mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amepongeza uteuzi huo.

Mgeja ambaye ni mmoja wa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa mkoa wa chama hicho ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jana.

Amesema yeye binafsi na wapenda maendeleo wengine mkoani Shinyanga wana kila sababu za kupongeza safu mpya ya mawaziri ambayo imeteuliwa na Rais Samia na kwamba wengi wao ni vijana ambao wako imara kiutendaji wakitokana na Chama cha Mapinduzi na wenye malezi na makuzi ya kiuongozi.

“Kwa kweli watanzania wengi hatuna mashaka na wateule wote hawa wapya na wale waliobakia wa zamani ni wachapakazi wazuri kikuba tuwatakie kila la kheri katika majukumu yao haya mapya waliyoaminiwa na Rais wetu,”

“Kikubwa tuwaombe wafanye kazi kwa juhudi na maarifa yaliyojaa weledi bila kusahau kuwa cheo ni dhamana hivyo wahakikishe katika utendaji wao wasije hawaiangushi mamlaka iliyowateua pamoja na watanzania, hususani Chama chetu cha Mapinduzi (CCM),” alieleza Mgeja.

Mwenyekiti huyo ambaye Taasisi yake hujishughulisha na masuala ya Haki, Demokrasia na Utawala bora amefafanua kuwa hatua ya kumpongeza Rais Samia kwa uteuzi wa mawaziri alioufanya inatokana na jinsi alivyoteuwa watu wanaoonesha wazi wameandaliwa kiuongozi tofauti na ilivyotaka kuzoeleka huko nyuma.

“Viongozi wanaandaliwa ndiyo maana sisi makada na wanasiasa wakongwe nchini tumeamua kuupongeza uteuzi huu kwa heshima kubwa kwani huko nyuma upatikanaji wa viongozi walioandaliwa ulianza kupotea mpaka ikafika tukawa tunapata viongozi ambao hawajaandaliwa kiuongozi,”

“Sasa utaratibu huu mara nyingi walioteuliwa walijikuta wakishindwa kutekeleza kikamilifu wajibu wao kwa wananchi hivyo ilikuwa ni hatari kubwa kwa Taifa kwa vile mbele ya safari kunaweza kukatokea ombwe kubwa la viongozi makini ambao hawajaandaliwa,” alieleza.

Aliendelea kueleza kuwa ilifika wakati baadhi ya wateule waliokuwa wakiteuliwa kujiona wao wana bahati ya “mtende” kiasi cha kulewa sifa na wengine kujinasibu kwamba wana bahati ya pekee ya kuteuliwa japokuwa waliokotwa majalalani.

Mgeja pia ametahadharisha na kuonya tabia ya baadhi ya watu kuwachafua vijana wazuri wachapa kazi inayofanywa na kundi la mahafidhina ambao kazi yao kubwa ni kuwachafua watu na kuwavunjia heshima huku wenyewe wakijipambanua eti ni wasafi kama malaika wakati ni wachafu sawa na shetani.

“Mchezo huu mchafu unaotokana na kundi au genge la mahafidhina ambao kazi yao kubwa ni kuwadhoofisha na kuwachafua vijana hasa wanapoona wanakuwa na mafanikio makubwa katika kuitumikia nchi yao, wao huwachafua ili waonekane hawafai, hii si tabia njema, lazima ikemewe,”

“Niwaombe tu watanzania wenzangu wenye mapenzi mema na nchi yao tushirikiane kwa nguvu zote na Serikali yetu iliopo madarakani hivi sasa, tuchape kazi na tutoe fursa kazi ziendelee kwa ajili ya maendeleo yetu, na niwashukuru wale wote wenye kumuunga mkono Rais Samia, tusikubali kuyumbishwa na wachache,” alieleza Mgeja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com