Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania Khamis Mgeja akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kada wa Chama cha Mapinduzi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation inayojihusisha na masuala ya haki, utawala bora na demokrasia Khamis Mgeja ameshauri jina la Job Ndugai liondolewe kwenye Soko Kuu la Dodoma kwa sababu bango hilo litaleta kichefu chefu kikubwa kwa watanzania.
Mgeja ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga amesema Job Ndugai hakuidharau tu Ikulu, hakumdharau tu na kumkejeli Rais Samia Suluhu Hassan bali aliwadharau Watanzania wote kwani unapomgusa Rais umewagusa Watanzania na Watanzania hawatapenda hata kuona hilo bango la Job Ndugai lililopo katika Soko Kuu la Dodoma.
“Kwa makosa hayo aliyoyafanya Ndugai kwa kweli hata kama kutakuwa na kumbukumbu zake zilizoandikwa ziondolewe. nchi zingine hata mabango, sanamu za viongozi wanaofanya mambo ya hovyo huwa zinaharibiwa na wananchi lakini kwa sababu sisi ni wastaarabu mimi nashauri hata lile Soko la Dodoma lililopewa jina la Ndugai niiombe serikali lile bango liondolewe kwa sababu litaleta kichefu chefu kikubwa kwa sababu Ndugai alidhalilisha nchi, aliwadhalilisha Watanzania”,ameongeza Mgeja.
“Ndugai alibeza juhudi za Rais Samia katika kuwaletea maendeleo Watanzania hali iliyosababisha wote tupate mashaka na hatukuamini hayo maneno yanaweza kutolewa na ndugu yetu Ndugai. Lakini inawezekana kuna tatizo la kiafya au ulevi wa madaraka lakini Waswahili wanasema ukilikoroga basi baadae unalinywa mwenyewe, kwa hiyo uamuzi huu aliochukua wa kujiuzulu ni uamuzi tuliotarajia wengi kwamba hana namna kwa sababu presha ya wananchi, nguvu za umma kila kona zilikuwa zikitaka kumshinikiza ajiuzulu, viongozi wenzake, wabunge wenzake, viongozi wa dini na wananchi kada mbalimbali”,ameeleza Mgeja.
Mgeja amewataka walio nyuma ya Job Ndugi wajitathmini haraka na wao wachukue hatua kama alivyofanya Nahodha wao Job Ndugai ya kujiuzulu na wajiuzulu ili kazi ziendelee nchini.
Yaliyopita si ndwere na sasa tugange yajayo lile genge lililobaki lenye mitazamo ya 2025 basi wajitathmini kama alivyosema Mhe. Rais kwamba wapishe waende na harakati zao wamuache Rais afanye kazi za kuwatumikia Watanzania na wote tumesema tunamuunga mkono Mama kwa nguvu zetu zote”,amesema Mgeja.
Social Plugin