Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGODI WAPONEA CHUPUCHUPU KUPIGWA FAINI KUBWA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Suleiman Jafo, akikagua Nyaraka zinazohusiana  na usafi na utunzaji wa  mazingira katika eneo la Mgodi wa Katavi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Suleiman Jafo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Katavi na Mgodi wa Katavi

Na William Budoya - Katavi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Suleiman Jafo, ameiagiza Kampuni ya Mgodi, Katavi (Katavi Mining CO. Ltd ) kushughulikia kwa haraka upatikanaji wa Cheti cha Mazingira na Uwepo wa Mfumo wa Majitaka (TSF) ndani ya mwaka 1 kuanzia Januari 2022.

Mhe. Jafo ametoa agizo hilo jana baada ya kufanya ukaguzi katika Kampuni ya Mgodi Katavi, na kugundua kuwa mgodi huo unaendesha shughuli zake bila cheti cha mazingira ambacho walipaswa kuwa nacho kabla ya kuweka miundombinu mbali mbali katika eneo la mgodi.

“Hapa kuna changamoto ya kimazingira kwa sababu mgodi hauna cheti cha mazingira wala mfumo wa majitaka(TSF), hivyo kutokuwepo kwa vigezo hivyo 2 vya usafi na utunzaji wa mazingira katika eneo la mgodi, ni kosa na uchafuzi wa mazingira, Mgodi unapaswa kutozwa faini kubwa.” Mhe. Jafo amesema.

Kufuatia mapungufu hayo, kiongozi huyo ameuagiza uongozi wa Mgodi kufanya marekebisho ya dosari hizo na kukamiisha ndani ya mwaka 1 kuanzia Januari 2022 hadi Januari 2023.

Mhe. Jafo ameonya kuwa kutokuzingatiwa kwa vigezo hivyo, kuna athari za uchafuzi wa mazingira ikiwemo kuchafua vyanzo vya maji na taka sumu kwenda kwenye ardhi jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine.

Kaimu Mtendaji wa Kampuni ya Mgodi, Katavi Mining CO. Ltd Bw. Twalib Mohamed amesema yeye pamoja na uongozi wa Mgodi, watatekeleza kwa haraka sana maagizo yote yaliyotolewa na waziri mwenye dhamana ya Mazingira nchini Tanzania ili kuendana na matakwa ya sheria ya mazingira.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko amemhakikishia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. S. Jafo, kuwa yeye na viongozi wenzake wataendelea kuwasimamia na kuwahimiza wawekezaji wote katika mkoa wake kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia mazingira.

Mhe. Jafo amewapongeza wawekezaji wa Kampuni ya Mgodi, Katavi kwa uwekezaji mkubwa katika nchi ya Tanzania, kwa kutengeneza ajira kwa watanzania,kuipatia serikali ya Tanzania mapato yake na kutoa michango mbali mbali kwa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com