Picha ya nguo ya ndani ya mwanamke haihusiani na habari hapa chini
Na Amiri Kilagalila, Njombe
Tyson Kilasi (32) mkazi wa Kijiji cha Mawindi halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, amekutwa amefariki kwa kujinyonga kwenye goli la uwanja wa mpira wa miguu wa uliopo kijijini hapo huku pembeni akiwa ameacha nguo ya ndani ya kike.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mawindi, Kata ya Igima bwana Elias Mwinami amethitibitisha kutokea kifo cha kijana huyo kilichotokea usiku wa kuamkia leo Januari 18, 2022.
Mwinami amesema chanzo cha kifo cha kijana huyo bado hakijafahamika ambapo eneo ambalo mwili wa kijana huyo wameukuta ni eneo la goli la mpira wa miguu na wamekuta nguo ya ndani ya mwanamke.
“Tumemkuta asubuhi ananing’inia kwenye goli lakini chanzo bado hakijafahamika na kimsingi tunalaani kitendo hiki ifike mahali tuelimike na hivi karibuni tu polisi walikuja kutoa elimu kwa kweli wananchi waache kujichukulia sheria mkononi,” alisema Mwinami.
Akizungumza kwa njia ya simu Diwani wa kata ya Igima bi. Paulina Samata Mwinami amesema kata ya Igima inahitaji juhudi za pamoja kuelimisha wananchi juu ya kuacha kujichukulia sheria mkononi na kwamba tukio hilo ni la pili kutokea kwenye kata hiyo.
Bi. Mwinami amesema wiki moja imepita mwanaume mmoja na mwanamke mmoja walikutwa wameuawa katika misitu ya kampuni ya Tanwat ambao walitambulika kuwa ni wakazi wa kata ya Igima mmoja wa kijiji cha Mawindi na mwingine mkazi wa kijiji cha Mhaji ambao uchunguzi wa polisi bado unaendelea.
“Nilivyojaribu kuuliza kama jana ulitokea ugomvi wamesema hawaelewi kwa kweli ninajiskia vibaya mno kwasababu watu sasa wanajichukulia sheria mkononi.Niombe wananchi kama wanakuwa na kitu ni vema wawe wanakitoa kuliko kuchukua uamuzi wa kujiua,” alisema Paulina Samata.
Baadhi ya wananchi na majirani wa marehemu huyo wamesema serikali iongeze kasi ya kuelimisha wananchi kupitia mikutano ili kupunguza matukio ya vifo katika kata hiyo na kwamba migogoro katika familia, ardhi na uhusiano wa kimapenzi ndiyo inayohisiwa kuwa chanzo cha matukio hayo.
Social Plugin