Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameanza ziara ya siku mbili katika Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro yenye lengo la kukagua miradi ya maji sambamba na kuwatambulisha Wakandasi watano waliochaguliwa kutekeleza miradi ya maji katika Wilaya hiyo.
Miradi hiyo mitano ni Misegese, Itete Njiwa, Igawa, Ngoheranga na Uchimbaji wa visima virefu 14 ambapo utekelezaji huo utagharimu jumla ya Shilingi Bilioni 2.8. Katika miradi hiyo mitano, mradi wa maji Ngoheranga unatekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 kiasi cha Shilingi Milioni 641.
Mahundi amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya shilingi bilioni tatu zitatumika kwa ajili ya miradi mbalimbali katika Wilaya ya Malinyi.
Ushirikiano baina yake na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na watumishi wa Wizara ya maji utaifanya Serikali kufikia malengo yake kwa nia ya kuwaondolea kadhia ya upatikanaji wa majisafi na salama.
Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha nyingi katika miradi ya maji ilu kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata majisafi, salama na ya uhakika hii ni katika kutimiza ile azma ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Malinyi Mheshimiwa Antipas Mgungusi mbali ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maji kwa ujumla amewatoa hofu wananchi kwa namna walivyokumbukwa katika miradi mbalimbali ya maji hivyo wananchi kuendelea kuiamini Serikali.
Mhe. Mgungusi hakusita kuwapongeza Mawaziri na watumishi wote wa Wizara kwa namna wanavyochukua hatua za kusimamia utekelezwaji wa miradi ya maji nchini.