Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NECTA YAFUTA MATOKEO YA WATAHINIWA WALIOFANYA UDANGANYIFU...YAZUIA MATOKEO YA WANAFUNZI 555


 NA GODFREY NNKO


BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 102 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani ya kidato cha nne uliofanyika mwishoni mwa 2021 huku udanganyifu ukiongezeka tofauti na mwaka 2020.



Katibu Mkuu wa NECTA, Dkt. Charles Msonde ameyasema hayo leo Januari 15,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 

“Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu watahiniwa 83 ni wa Upimaji wa kitaifa wa darasa la nne, 27 ni wa upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili, 102 ni wa mtihani wa kidato cha nne na watahiniwa wawili ni wa mtihani wa maarifa,” amesema Dkt. Msonde.

Ikilinganishwa na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2020, mwaka huu wanafunzi wengi zaidi waliohusika kufanya udanganyifu kwenye mitihani ya kidato cha nne ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 27.

Mwaka jana, ni wanafunzi 75 tu ndiyo walifanya udanganyifu katika mtihani huo.

Baraza hilo limesema limefuta matokeo ya wanafunzi hao kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) na (j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) 2016 cha Kanuni za Mitihani.

NECTA pia imezuia matokeo ya wanafunzi 555 ambao walipata matatizo ya kiafya na hivyo kushindwa kufanya mitihani yote au baadhi.

“Watahiniwa wahusika wamepewa fursa nyingine ya kufanya upimaji wa mtihani hii ya kitaifa mwaka huu wa 2022,” amesema Dkt.Msonde.

Amesema, kati ya watahiniwa 483,820 wasichana waliofaulu 218,174 sawa na asilimia 85.77 huku wavulana wakiwa 204,214 sawa na asilimia 89.00 wamefaulu.

“Mwaka 2020 watahiniwa 373,958 sawa na asilimia 85.84 wa shule walifaulu mtihani huu. Hivyo ufaulu wa watahiniwa wa shule umeongezeka kwa asilimia 1.46 ikilinganishwa na mwaka 2020,” amesema.

Dkt. Msonde amesema, katika matokeo hayo Shule ya Kemebos ya Kagera imeshika nafasi ya kwanza katika 10 bora kitaifa ikifuatiwa na shule za St. Francis (Mbeya), Waja (Geita), Bright Future Girls (Dar es Salaam) Bethel Sabs Girls (Iringa), Mau Seminary (Kilimanjaro) na Feza Boys’ (Dar es Salaam).

Shule nyingine ni Precious Blood ya Mkoa wa Pwani, Feza Girls’ (Dar es Salaam) na Mzumbe ya mkoani Morogoro.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com