Katibu Mtendaji, Baraza la Mitihani la Tanzania anapenda kuwajulisha watu wote wanaotarajia kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) Novemba, 2022 kama Watahiniwa wa Kujitegemea kwamba; 1. Kipindi cha kawaida cha Usajili kitaanza tarehe 01/01/2022 kwa ada ya Shilingi 50,000/= kwa wanaojisajili CSEE na Shilingi 30,000/= kwa wanaojisajili QT na kitaishia tarehe 28/02/2022.
Aidha, watakaojisajili kwa kuchelewa kuanzia tarehe 01/03/2022 hadi tarehe 31/03/2022 watalipa Shilingi 65,000/= kwa Watahiniwa wa Kidato cha Nne (CSEE) na Shilingi 40,000/= kwa Watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa (QT) ikiwa ni ada ya kawaida pamoja na faini.
2. Mtahiniwa atakayejisajili kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2022 ni yule ambaye anarudia Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) au amefanya na kufaulu Mtihani wa Maarifa (QT) katika kipindi kisichozidi miaka mitano (5) iliyopita au mwenye sifa zinazolingana na hizo alizopata kutoka nje ya Nchi na kufanyiwa ulinganifu na Baraza la Mitihani la Tanzania.
3. Mtahiniwa atakayejisajili kufanya Mtihani wa Maarifa ni yule ambaye anatafuta sifa ya kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne kama Mtahiniwa wa Kujitegemea.
4. Usajili unafanyika kwa njia ya mtandao, kwa kufuata hatua zifuatazo; (a) Fika Kituo utakachofanyia Mtihani ili kupata namba rejea (Reference Number) ambayo inatolewa bure. (b) Fika Ofisi ya Posta kupata ‘Control Number’ ya kufanyia malipo ya ada ya Mtihani au ingia katika tovuti ya Baraza la Mitihani ili utengeneze ‘Control number’ ya kufanyia malipo kwa utaratibu ulioelekezwa. (c) Fanya malipo ya ada ya Mtihani kupitia Posta au Benki kwa kutumia ‘Control Number’. (d) Fika Posta kufanya usajili au jisajili mwenyewe kupitia tovuti ya Baraza la Mitihani kwa kufuata hatua zilizooneshwa kwenye tovuti. (e) Baada ya usajili kukamilika chapa na wasilisha nakala moja ya fomu Ofisi ya Posta, wasilisha nakala ya pili kwenye Kituo utakachofanyia Mtihani na nakala ya tatu ya fomu itunzwe na wewe (mtahiniwa) mwenyewe kwa ajili ya kumbukumbu.
5. Ufafanuzi kuhusu utaratibu wa hatua za kufuata katika usajili, umetolewa katika tovuti ya Baraza la Mitihani www.necta.go.tz. Waombaji wote wanasisitizwa kuhakikisha wanajisajili mapema kwani mfumo wa usajili utafungwa baada ya kipindi cha usajili kumalizika.
Imetolewa na; KATIBU MTENDAJI
Social Plugin