KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco raia wa Hispania amefichua kuwa hawajaenda kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kama washiriki wa michuano kwa kuwa malengo yao ni kuhakikisha wanachukua ubingwa wa kombe hilo kutokana na ukubwa wa timu yao.
Pablo ametoa kauli hiyo kabla ya leo Jumatano, Simba kucheza mchezo wake wa kwanza katika michuano hiyo dhidi ya Selem View saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Akizungumza na Championi Jumatano, Pablo alisema: “Malengo makubwa ni kuona katika michuano hii tunaweza kuchukua ubingwa hilo ndiyo jambo kubwa ambalo limetuleta huku kwa sababu hatukuja kama washiriki wa haya mashindano bali tumekuja kama moja kati ya timu washindani ambao tunahitaji kuona tunaondoka na ubingwa.
“Nimeambiwa msimu uliopita hatukuweza kufikia malengo kwa sababu tulifungwa na wapinzani wetu Yanga kwenye mchezo wa fainali lakini safari hii naamini tumekuja na timu ambayo inaweza kupata matokeo katika mchezo wowote hadi kufikia malengo yetu na ndiyo ambalo tunaliangalia kupata ushindi kwenye kila mechi ambayo itakuwa mbele yetu.”
STORI: IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam