Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Tanzia : DIWANI WA KATA YA MWAMALILI PAUL MACHELA AFARIKI DUNIA


Paul Machela  enzi za uhai wake

**
Diwani wa Kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga Paul Machela (CCM) amefariki dunia leo Januari 1,2022 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhani Masumbuko amesema Paul Machela amefariki dunia leo majira ya saa 11 alfajiri wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa zaidi ya wiki moja.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha diwani mwenzetu Paul Machela. Ameacha pengo kubwa kwani alikuwa na mchango mkubwa katika mipango ya maendeleo ya Manispaa ya Shinyanga. Alikuwa mshiriki mkubwa katika mipango mikubwa tuliyokuwa tumejiwekea katika Manispaa ya Shinyanga”,amesema Masumbuko.

“Mpendwa wetu Paul Machela alikuwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa zaidi ya wiki moja kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu na Moyo kuzungukwa maji. Desemba 29,2021 hali yake ilibadilika akapelekwa katika chumba maalumu cha uangalizi (ICU),taarifa za madaktari jana usiku alikuwa anaendelea vizuri lakini leo saa 11 alfajiri hali ilibadilika akafariki dunia. Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Paul Machela. Amina.”,amesema.

Paul Machela amekuwa diwani wa kata ya Mwamalili kwa zaidi ya miaka 15,mwaka huu 2022 alikuwa anatimiza miaka 17 ya kutumikia kiti cha udiwani.

Machela ana historia ya kuwa Diwani asiyeyumbishwa kwenye msimamo au hoja zake na atakumbukwa 
kwa kusimamia ukweli na amehudumu kama Diwani wa kata ya Mwamalili kwa muda mrefu na wananchi wake walimpenda.

R.I.P Paul Machela

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com