Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi,ACP Ali Hamad Makame
Na Walter Mguluchuma -Katavi
Kijana mmoja mkazi wa Kijiji cha Mtisi Kata ya Sitalike Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi aliyefahamika kwa jina la Baraka Said Kabisu (30) ameuawa kikatili kwa kupigwa na silaha za jadi na kitu chenye uzito mkubwa na ncha kali na kundi la watu wenye hasira kali baada ya kutuhumiwa kwa ushirikina wa kutengeneza radi iliyompiga Angelina Levocatus Kifua(16) Mkazi wa kijiji hicho .
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ali Hamad Makame amesema tukio hilo la mauaji limetokea Januari 24,2022 majira ya saa 12 jioni kijijini hapo baada ya taarifa za kifo cha Angelina kuwafikia majira ya saa kumi na mbili jioni Kijiji hapo.
Ndipo kundi kubwa la wananchi lilijikusanya huku wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na baada ya kuwa wamekunyika kundi hilo liliamua kwenda nyumbani kwa marehemu huyo kwa lengo la kumshambulia kwa kumtuhumu kuwa ni mchawi aliyetengeneza radi iliyompiga na kumuua mwanakijiji mwenzao .
Kamanda amesema kuwa baada ya kuwa wamefika nyumbani kwake walimshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa silaha za jadi na kupelekea kifo chake ambapo walimpiga kwenye paji la uso na kisogoni.
Wananchi hao baada ya kuwa wamefanya mauaji hayo ya kikatili kwa marehemu huyo waliyemtuhumu kuwa mchawi aliyetengeneza radi iliyouwa mwanakijiji mwenzao walitokomea kusikojulikana.
Aidha Kamanda ameeleza kuwa watuhumiwa nane wa tukio hilo tayari wamekamatwa na wanaendelea kuwahoji na wengine ambao watatajwa kuhusika na mauaji hayo wataendelea kuwakamata na uchunguzi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa juu yao.
Kamanda Makame ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kuacha tabia ya kuamini mambo ya kishirikina kwani kuna mambo mengine yanayotokea uasili wake ni ya kimungu wala sio ya kibinadamu yapo mambo ya kimungu wamwachie Mungu mwenyewe.
Amesisitiza Jeshi la Polisi wataendelea kuwakamata watu wote wanaokiuka taratibu za sheria ya nchi kwani kila mtu ana haki ya kuishi na kuendesha maisha yake kwa kuzingatia kanuni na taratibu hizo.
Chanzo - Katavi Press Club Blog