Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihutubia Taifa kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari Wakati alipokua akitoa Salamu za Mwaka Mpya leo tarehe 31 Desemba 2021.
PICHA NA IKULU
*********************************************
Ndugu Wananchi na Watanzania wenzangu;
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema na Huruma, kwa kutujaalia uhai na afya, na kutuwezesha kuumaliza Mwaka 2021 kwa amani na kuushuhudia Mwaka Mpya wa 2022 ukiingia. Wapo wapendwa wetu wengi ambao tungelipenda kuwa nao katika kipindi hiki cha furaha, lakini hatupo nao. Tuwaombee wapendwa wetu hawa Mungu aendelee kuwalaza mahali pema peponi. Amina.
Kwa wale ambao tumeendelea kubarikiwa tunu hii ya uhai basi hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu. Ni wazi kuwa katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka wengi wetu hupenda kutumia muda huu kufanya tathmini ya malengo yetu tuliyojipangia katika kipindi cha mwaka wa kalenda uliopita, ikiwa ni pamoja na kusherehekea mafanikio tuliyoyapata. Hivyo, ni katika msingi huo, nimeona ni vyema nami nikaongea nanyi ili kwa pamoja tuweze kufanya mapitio ya mwaka 2021 na kutathmini milima na mabonde tuliyopitia kama Nchi na Taifa, katika mwaka huo.
Ndugu Wananchi na Watanzania wenzangu;
Safari yetu ya Mwaka 2021 haikuwa tambarare; ilikuwa na milima na mabonde, furaha na majonzi, na mafanikio na vikwazo kadhaa. Huu ni mwenendo wa Maisha, huwezi kupata na kufurahia mafanikio bila kukutana na vikwazo vya hapa na pale. Msemo huu ulisadifu safari yetu ya 2021 kama Taifa. Pamoja na kupiga hatua kimaendeleo katika maeneo mbalimbali, tulikumbana pia na vikwazo na vipindi vya majonzi.
Mwaka 2021 Taifa letu lilipitia katika kipindi kigumu kwa kumpoteza Kiongozi Mkuu wa Nchi, mpendwa wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, wakati akiwa madarakani; na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad. Hakika ilikuwa ni misiba mikubwa kwa Taifa na Bara la Afrika kwa ujumla. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tuliweza kuwapumzisha wazee wetu hawa kwa amani. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwalaza mahali pema peponi. Amina.
Mwaka 2021, tuliendelea kukabiliana na janga la UVIKO – 19, ambalo linaendelea kuisumbua dunia hadi hii leo. Janga hili lilisababisha kuzorota kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, kutoka ukuaji wa asilimia 7 mwaka 2019/2020 hadi asilimia 4.8 mwaka 2020/2021. Kupungua kwa kasi ya ukuaji uchumi kulitokana na mambo mawili makubwa. La kwanza, ni athari za kufungwa mipaka, kusitishwa safari za ndege za kimataifa na kusitishwa baadhi ya shughuli za uzalishaji na kiuchumi. Hatua hizi zilichukuliwa na mataifa ambayo kati yao, ni washirika wakubwa wa biashara na Tanzania, kwa lengo la kukabiliana na janga la UVIKO – 19. La pili, ni mvua zilizozidi wastani ambazo zilisababisha uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji nchini na kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi.
Aidha, kuelekea mwishoni mwa mwaka 2021, tulishuhudia mfumuko wa bei uliofikia asilimia 4.1, kiwango ambacho kipo ndani ya malengo ya Taifa ambacho ni asilimia 3 hadi 5. Mfumuko huo wa bei ulisababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta duniani; na mlipuko wa UVIKO-19 ambapo viwanda vingi vilisimamisha uzalishaji na hivyo kusababisha uhaba na ongezeko kubwa la uhitaji wa bidhaa. Kwa hapa nchini mfumuko huo wa bei ulichagizwa zaidi na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 uliotoa kiasi cha Shilingi trilioni 1.3, kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya afya, elimu, maji safi na salama ambao ulisababisha upandaji wa bei za vifaa vya ujenzi kama Saruji, Nondo, Mabati.
Ndugu Wananchi na Watanzania Wenzangu;
Pamoja na vikwazo nilivyovitaja hapo juu ambavyo tulikumbana navyo katika Mwaka wa 2021, Watanzania tulipata mafanikio katika nyanja mbali mbali. Miongoni mwa maeneo ambayo tunapaswa kujivunia na ambayo nimeona ni muhimu niyataje ni pamoja na; kuweza kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu; kulikoendana na kuendeleza umoja, mshikamano na upendo miongoni mwetu. Mtakumbuka kwamba kwenye hotuba yangu ya kwanza niliyoitoa baada ya kuapishwa, niliwaomba na kuwasihi sana Watanzania, tuwe watulivu, na tudumishe umoja na mshikamano. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Watanzania kwa kudumisha Amani na Utulivu nchini na hatimaye, Taifa letu likibaki kuwa salama na imara.
Eneo jingine ambalo tuliweza kupata mafanikio katika Mwaka 2021 ni kuwa, pamoja na athari za UVIKO-19 tulikuwa na ukuaji chanya wa uchumi, tukiwa ni miongoni mwa nchi 11 zilizokuwa kiuchumi kati ya nchi 54 za Afrika. Hali hii ilisababishwa na kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kiuchumi badala ya hatua za kuwafungia kama ilivyokuwa kwa nchi nyengine.
Aidha, katika kuhakikisha uchumi haupati athari hasi, tulichukua hatua za kudhibiti Mfumuko wa bei, ambapo umeendelea kuwa kati ya asilimia 3 hadi 5; na kuhakikisha kwamba tunakuwa na akiba ya kutosheleza ya fedha za kigeni ambapo kwa sasa nchi yetu ina kiwango cha kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 6,253 zitakazotosheleza kuagiza chakula na huduma kwa kipindi cha miezi 7.
Vilevile, katika kuvutia uwekezaji na kurudisha fedha kwenye mzunguko, tulifanya marekebisho mbalimbali ya Kisera, kisheria, kikodi na kiutendaji. Matokeo yake tumeweza kuvutia uwekezaji kutoka miradi 186 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 1.013 mwaka 2020 hadi miradi 237 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 4.144 mwaka 2021.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kilimo, tulifanikiwa kuiongezea uwezo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa kuipatia mtaji wa Shilingi bilioni 208 ili iweze kuwafikia wakulima zaidi na kufanya kazi kwa ufanisi. Aidha, tuliweza kuondoa vikwazo vya biashara vilivyokuwepo na kuanzisha masoko na kufungua vituo vya kuuza mazao katika nchi za Kenya, Sudan Kusini, China, India, Ukraine, Umoja wa Ulaya, nchi za ukanda wa SADC na Saudi Arabia. Vilevile, Serikali iliziwezesha Ghala la Taifa la Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CBP) kununua tani 950,000 za mahindi zilizokuwa mikononi mwa wakulima.
Pamoja na mafanikio hayo katika sekta ya Kilimo, tunatambua uwepo wa changamoto ya upungufu wa mbolea, ambayo kwa kiasi kikubwa imesababishwa na kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa hiyo duniani kwa sababu ya UVIKO-19. Lakini habari njema ni kwamba, mapema mwakani 2022 tunatarajia kupata mbolea ya kukuzia mazao itakayouzwa kwa bei ambayo wakulima wameizoea. Pamoja na jitihada hizo, Kampuni ya ITRACOM Fertilizers Ltd, inajenga kiwanda kikubwa cha mbolea Jijini Dodoma, ambacho kitazalisha tani 500,000 sawa na takriban asilimia 70 ya mahitaji yetu kwa mwaka. Aidha, Kampuni ya Dangote nayo imeonesha nia ya kuanzisha Kiwanda cha Mbolea ya UREA kule Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Sekta ya Utalii nayo iliathiriwa sana na UVIKO-19, hatua mbalimbali za kuinusuru sekta hii kutodidimia zilichukuliwa na kuhakikisha sekta inarudi kwenye nafasi yake ya kuchangia uchumi wetu. Hadi mwezi Desemba mwaka huu 2021, sekta hii imeweza kujikongoja na kuingiza nchini Watalii 1,400,000 ikilinganishwa na watalii 620,867 kwa kipindi cha mwaka 2020, sawa na ongezeko la watalii 779,133. Matarajio yetu ni kushuhudia kukua zaidi kwa sekta hii kuanzia msimu wa 2022, na kuendelea.
Aidha, mwaka 2021 tuliendelea na utekelezaji wa miradi yetu mikubwa ya kimkakati, ikiwemo mradi wa ufuaji umeme wa Nyerere kule Rufiji; upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam; ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi kule Mwanza, daraja la Tanzanite Dar es Salaam; upanuzi wa barabara za viwanja vya ndege yaani Run ways, na Barabara kadhaa zinazounganisha Mikoa na Wilaya ya nchi yetu. Lakini vilevile ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ambapo tarehe 28 mwezi huu tumesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha tatu cha kutoka Makutupora hadi Tabora chenye kilometa 368.Pia, tumefanikiwa kuongeza ndege nyingine tatu (03), ambazo ni Dash 8 Q-400 ndege moja na Airbus 200 dege mbili, na kulifanya Shirika letu la ATCL kuwa na ndege 12.
Vile vile, tumeendelea na ujenzi wa Makao Makuu ya Nchi yetu Dodoma, ambao unahusisha ujenzi wa Ikulu ya Chamwino uliokamilika kwa asilimia 90, na tumeanza awamu ya pili ya ujenzi wa Mji wa Serikali pale Mtumba. Kwa ujumla Makao Makuu Dodoma yanaendelea kujengwa na Serikali na Sekta binafsi kwa kasi ya kuridhisha.
Halikadhalika, katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na mazingira mazuri ya kisiasa, Baraza la vyama vya Siasa Tanzania limekutana na wadau mbalimbali wa siasa na demokrasia na kujadili kwa pamoja mustakabali na namna bora ya uendeshaji wa siasa za vyama vingi nchini kwetu. Matumaini yangu ni kwamba kikosi kazi kilichoundwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kitafanyia kazi maazimio ya mkutano huo kwa weledi. Serikali itapokea mapendekezo yatakayoletwa na tuone hatua za kuchukua ili tuweze kusonga mbele kwa pamoja, kama Taifa.
Ndugu Wananchi;
Kwenye Uhusiano wa Kimataifa tumeweza kuifungua nchi yetu kwenye uwanda mpana wa ushirikiano na uhusiano, na kutuwezesha kuimarisha sauti yetu na ushawishi wetu kimataifa.
Aidha, mwaka 2021 Nchi yetu ilipata heshima kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) kuitangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. Hii ni hatua nzuri ya kufikia lengo la kukifanya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zitakazotumika na Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wa Sanaa, Michezo na Utamaduni, tunajivunia vijana wetu wa Tembo Warriors kwa kufuzu kushiriki katika Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu litakalofanyika mwezi Oktoba mwakani 2022 kule nchini Uturuki. Vile vile Timu ya mpira wa miguu ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) tunawapongeza kwa kubakiza hatua moja ya kushiriki kombe la Dunia kule nchini Costa Rica na Mungu awasaidie wapate sifa ya kwenda huko; na Warembo na watanashati wetu viziwi ambao watashiriki mashindano ya Dunia kule Brazil nao pia tunawapongeza. Haya ni mafanikio makubwa kwetu katika medani ya michezo. Ni fakhari kwetu pia kuona vijana wetu wa tasnia ya muziki wameweza kushiriki na kupata tuzo mbalimbali katika ngazi za kimataifa. Kwa ujumla tumeshuhudia ukuaji katika sekta ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kuelezea kwa uchache changamoto na mafanikio yetu kwa mwaka 2021, sasa nizungumzie kwa kifupi masuala mtambuka wakati tukiuelekea Mwaka 2022. Serikali inautizama mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa kukabiliana na changamoto zinazopunguza uwezo wa Wananchi katika kukabiliana na Maisha ya kila siku. Kama ilivyotamkwa kwenye Mpango wa Tatu wa Serikali wa Miaka Mitano wa 2021/2026, kwamba lengo kuu ni kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, kama nilivyosema hapo awali, dunia bado inakabiliwa na UVIKO – 19 na kwa sasa tupo katika wimbi la nne la ugonjwa huo. Kirusi kipya cha Omicron kinaenea kwa kasi kubwa, na tayari kipo na kimeshaingia nchini kwetu. Niwakumbushe kuchukua tahadhari kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya. Pia, nitumie fursa hii kuwahimiza wananchi kupata chanjo dhidi ya UVIKO – 19. Natambua kuwa chanjo haizuii mtu kupata maambukizi, ila inapunguza makali ya ugonjwa huo. Hivyo niwahimize wananchi kwenda kuchanja. Chanjo zipo na zinapatikana bila malipo.
Vile vile, mwaka 2022 ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi, hivyo naendelea kuwahimiza Watanzania kujitokeza kuhesabiwa ili tuweze kupata Takwimu zitakazotusaidia katika kupanga kwa usahihi masuala yetu ya maendeleo.
Halikadhalika, kwa watumishi wote wa umma na sekta binafsi, nitoe rai kuwa ni vyema tukauanza mwaka mpya wa 2022 na lengo la kuongeza ufanisi katika uzalishaji na ubora katika utoaji wa huduma. Tuazimie kuinua uchumi na kustawisha hali zetu, na tuendelee kulipa kodi stahiki kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Kwa wazazi wenzangu, nawasihi msijisahau na tafrija na sherehe za Sikukuu; ni vyema mkatumia muda huu kuwaandaa watoto wetu kukabiliana na changamoto mpya za kimasomo, na kuhakikisha kwamba hawaikosi fursa adhimu ya elimu bila malipo inayotolewa na Serikali yao.
Ndugu Wananchi;
Ni utamaduni na desturi kuwa kipindi hiki cha Sikukuu za mwisho wa mwaka huwa tunatumia muda huu kuwatembelea wazazi, ndugu, jamaa na marafiki katika maeneo mbalimbali. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwakumbusha wale watakaokuwa safarini kurudi kutoka maeneo mbalimbali ambayo walikwenda kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka, kuzingatia na kuheshimu sheria za barabarani ili kupunguza ajali zinazoepukika ambazo mara nying humaliza nguvu kazi ya Taifa.
Kwa kumalizia, napenda kuwatakia Watanzania wote kheri, fanaka na mafanikio katika Mwaka wa 2022. Tuombe Mwenyezi Mungu atushushie Neema na Baraka na atunusuru na kila aina ya majanga ndani ya nchi yetu. Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie Afya, Siha na Nguvu, na atujaze hekima, busara na uadilifu katika kuliendeleza Taifa letu. Aamiin, Aamiin.
Kwa mara nyingine tena, nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwatakia Kheri ya Mwaka Mpya wa 2022.
Ahsanteni sana.
Social Plugin