Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MTAKA AAPA KUWANYOOSHA WAZAZI WENYE WATOTO WATORO


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akiongea na wazazi,walezi,walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Zuzu Jijini Dodoma
Picha ya pamoja kati ya wanafunzi wa Shule ya sekondari Zuzu na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka alipotembelea shuleni hapo kutafuta namna ya kupandisha kiwango cha ufaulu kutokana na shule hiyo kushika nafasi ya 51 kati ya shule 52 za Mkoa wa Dodoma.
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1blog, DODOMA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amewaagiza watendaji wa Mitaa mitano katika Kata ya Zuzu Jijini Dodoma kuwatafuta na kuwakamata wazazi na walezi wa watoto 88 ambao hawajaripoti masomo ya kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Zuzu tangu shule zifunguliwe Januari 17 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa Mtaka ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wazazi, walezi, walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Zuzu kuhusu namna ya kuboresha ufaulu shuleni hapo ambapo katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana 2021 ilishika nafasi ya 51 kati ya shule 52.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma, alisema wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapaleka watoto wao shule mpaka ifikapo Jumatatu ya wiki ijayo wakamatwe na kupewa kazi ya kufanya usafi katika shule pamoja na katika miradi ya Serikali ambayo inaendelea kujengwa Mkoani hapa.

Alisisitiza kuwa wazazi na walezi hao kwa nyakati zote wanapaswa kutoa kipaumbele katika elimu kwa kuhakikisha kuwa Watoto wao wanahudhuria masomo huku kwa wakati huku wakifuatilia mienendo yao na kuidhibiti ile isiyofaa ambayo inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu.

"Jumatatu ya wiki ijayo nitafanya msako wa nyumba kwa nyumba kujua ambao watakuwa wamekaidi agizo hili,nawaambia Magereza huwa haijai,"alisema 

"Na nyie watendaji wa mitaa ya Mazengo,Pinda,Sokoine,Soweto na Chididimo katika Kata ya Zuzu hakikisheni wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanafika shuleni haraka ili kuanza masomo mara moja,"alisisitiza

Alisema kwa kutumia migambo wanatakiwa kuwakamata wale wote ambao watakuwa wamekaidi agizo hilo ikiwa ni pamoja na kuwapa jukumu la kufanya usafi katika vyoo vya shule pamoja na katika miradi ya Serikali.

“Mzazi ambaye mwanae atakuwa hajaripoti shuleni akamatwe akasafishe vyoo huku watoto wakiwa wanaona ikiwezekana wawe vibarua katika miradi inayoendelea kujengwa na Serikali akiwa kapeleka mtoto wake Private simu ipigwe shuleni waulizwe,”alisema.

Alisema katika hilo hatanii na atalisimamia kwa nguvu zake zote huku akidai kwamba wale wote watakaofanya hivyo atahakikisha wanakimbia nyumba zao.

“Sitaki kusikia mtoto anabaki nyumbani anataka aje shule,kwangu mtaelewa kwanguvu na hapa ninamanisha sina utani katika hili hatuwezi kujenga nitahakikisha mpaka mnakimbia nyumba zenu sitaki utani katika hili,”alisema.

Aidha,RC Mtaka amesema atafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwatafuta wale wote ambao watakuwa wamekaidi agizo hilo huku akitaka kila mzazi kubeba jukumu lake.


Amewataka wazazi kuwasaidia wanafunzi waweze kutimiza ndoto zao za kusoma na kuacha kulalamika kwamba wanatembea umbali mrefu.

“Kila mzazi abebe hasira za kuhakikisha mwanae anasoma na kufaulu agenda ya elimu iwe kipaumbele kwa kila mmoja sitaki kusikia habari ya maneno maneno wanafunzi wanatakiwa kusoma,”alisema.


Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo ,Dismas Chilala amesema wanakabiliwa na changamoto ya uelewa wa wazazi na wanafunzi kuhusu umuhimu wa elimu kwani wengi wamekuwa hawamalizi shule kutokana na sababu mbalimbali.

“Hapa changamoto Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ni mtazamo wa elimu ni nini katika jamii na manufaa yake ni yapi,hapa wengi wanaoanza kusoma hawamalizi,”alisema

Kwa upande wake, Diwani Kata ya Zuzu,Awadh Abdallah alisema changamoto kubwa ambayo wanakutana nayo ni wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuchukuliwa na kwenda kufanya kazi za ndani pamoja na wengine kutokuripoti shuleni.

Alisema kunahitajika jitihada kuhakikisha wanafunzi wanaoonza kidato cha kwanza kuwasaidia mpaka wamalize kidato cha nne kwani wengi wamekuwa hawamalizi.

Pamoja na hayo alifafanua kuwa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wa kilomita 6 kutoka Chididimo hadi Zuzu aliitatua kwa kutoa nyumba ili wanafunzi waweze kukaa na kutakiwa watoe shilingi 15,000 kugharamia maji na chakula lakini wengi walikataa.

Kutokana na hayo mmoja wa walimu wa shule hiyo (hakutaka kutajwa)ameeleza kuwa shida hiyo ya ufaulu wa chini wa wanafunzi inatokana na mfumo unaotumika kuwachagua kujiunga na masomo ya sekondari.

Alishauri mfumo uliopo ubadilishwe kwani kuna baadhi ya wanafunzi wanapelekwa kujiunga na masomo ya sekondari wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.

"Inashangaza sana kuona tunaletewa wanafunzi hawajui hata kuandika majina yao ,wakati mwingine unajiuliza wamefikaje hapa,Ili kuondokana na shida hii ni lazima tuukubali ukweli kwamba tunapaswa kuwanyoosha hawa watoto kuanzia shule za msingi na hapo tutafanikiwa,"alieleza Mwalimu huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com