Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MTAKA AMUANDALIA ZAWADI RAIS SAMIA


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akiongea wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa soko la machinga Jijini hapa unaolenga kuboresha biashara .
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru akiongea na wataalamu wa ujenzi wa soko la machinga

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog, DODOMA.

MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka ameitaka Kampuni ya Mohammed Bulders inayojenga eneo la Wamachinga katika eneo la Bahirod Jijini hapa kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa mradi huo ifikapo Machi 17 mwaka huu.

Amesema mradi huo ukikamilika kwa wakati  itakuwa ni alama ya zawadi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kutimiza mwaka mmoja  tangu awe madarakani.

Mtaka ameeleza leo,Januari 13,2022 wakati alipofanya ziara katika eneo hilo ambapo amesema sababu ya kutaka ujenzi wa eneo hilo ukamilike March 17 ni kutokana na Rais Samia siku hiyo atakuwa anafikisha mwaka mmoja  akiwa madarakani.

“Mnajua sababu ya kutaka Marchi 13 muwe mmemaliza huu mradi ni kwamba siku hiyo Rais atakuwa anatimiza  mwaka mmoja akiwa madarakani hivyo nataka tumzawadie  zawadi ya soko kwa kuwa na yeye hataki wamachinga wapate shida,”amesema.

Pamoja na hayo Mkuu huyo wa Mkoa amesema atawashirikisha wataalamu wote kuhakikisha soko hilo linajengwa kisasa na linakuwa na mahitaji yote maalumu ikiwemo maji,vyoo,chakula na umeme.

“Tunahitaji ubora wa hali ya juu ndo maana wataalamu wote wapo hapa lengo langu tujenge kitu cha kueleweka,nataka Halmashauri zote 184 zije zijifunze hapa namna ya kujenga soko bora la wamachinga hapa kutakuwa na kila kitu na litakuwa soko la saa 24,”amesema.

Kadhalika  amelitaka Jiji la Dodoma  kuwaondoa wamachinga wote waliopo katikati ya Mji mara baada ya Soko hilo kukamilika lengo likiwa ni kuliweka Jiji katika hali ya usafi.

“Nategemea mara baada ya kukamilika kwa Soko hili,wamachinga wanaokaa mjini watatupisha na kuja katika hili eneo naamini hapa Mji utakuwa safi na mambo mengine yataenda vizuri,sitegemei soko liwe limekamilika halafu wamachinga wawe wanazagaa mjini,”amesema.

Kutokana na hayo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru ameahidi kusimamia ujenzi huo hadi utakapo kamilika  na kuhakikisha wamachinga wanakabidhiwa na kuanza biashara zao mara moja.

"Soko hili litakapo kamikika lina uwepo wa kupokea wamachinga 5000 japo tutaanza na wamachinga 3000 ambao tayari tumewasajili na tutaendelea kuwasajili wengine hadi kufikia idadi kamili,"amesisitiza Mafuru.

Mafuru ameuagiza pia uongozi wa machinga kuhakikisha wanasajili wamachinga pekee huku akitahadhalisha  wale wasio wamachinga waondolewee kwenye orodha ya usajili na kusisitiza kigezo cha kufanya biashara kwenye Soko hilo ni machinga na sio vinginevyo.

Hata hivyo Amesema mara baada ya soko kukamilika hatarajii kuona machinga yeyote katikati ya Jiji .

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma,Dk.Fatma Mganga ametumia nafasi hiyo kulipongeza Jiji la Dodoma kwa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kuweza kujenga eneo hilo la wajasiriamali kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 7 .

Dk.Mganga pia amezitaka Halmashauri nyingine za Mkoa huu  kuiga mfano wa Jiji la Dodoma.

"Hii ni hatua nzuri ,tunataka watu wetu wafanye biashara kwa uhuru nawaomba nyie mnaojenga kampuni ya Mohammed Builders kujenga eneo hilo kwa kiwango ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya kuweka mizigo na kufanyia biashara.

Katika ziara hiyo,Mkuu huyo wa Mkoa alikuwa ameongozana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma,Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma,Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa,wataalamu kutoka Jiji la Dodoma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com