SERIKALI YATANGAZA KUSHUKA KWA BEI ZA MAFUTA



Mamlaka ya Huduma za Udhibiti wa Nishati na Maji (EURA) imetangaza kushuka kwa bei za mafuta kwa mwezi Januari 2022 ikilinganishwa na bei za Desema 2021.

Kwa mujibu wa EWURA, bei za Januari 2022 zitapungua kwa kati ya shilingi 4 na 35 kwa lita ya petroli; na kati ya Shilingi 43 na 67 kwa lita ya dizeli isipokuwa kwa bandari ya Mtwara ambapo bei zitaongezeka kwa Shilingi 2 kwa lita; huku bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa Shilingi 99 kwa lita kama inavyoonekana katika Jedwali Na. 1.

Mamlaka hiyo imeeleza zaidi kwamba bei za mafuta zingepungua zaidi iwapo thamani ya dola ya Marekani isingeongezeka dhidi ya Shilingi ya Tanzania ambapo dola ya Marekani imenunuliwa kwa Shilingi 2,314.23 ikiwa ni ongezeko la thamani kwa asilimia moja kutoka Shilingi 2,300.88 kwa dola.

Uamuzi uliochukuliwa na serikali Oktoba 2021 wa kupunguza tozo za taasisi za Serikali kwa lengo la kupunguza bei za mafuta hapa nchini umesaidia kupunguza bei za mafuta kwa kati ya Shilingi 23 na Shilingi 31 kwa lita kwa kutegemea aina ya mafuta na bandari yalipopokelewa mafuta hayo.

Vilevile, kutokana na kuendelea kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia, Serikali iliahirisha ukusanyaji wa ada ya mafuta (petroleum fee) kuanzia Desemba 2021 na hivyo kufanya bei ya juu kufikiwa katika mwaka 2021 kuwa ni Shilingi 2,510 kwa lita ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam, Shilingi 2,525 kwa lita ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga na Shilingi 2,569 kwa lita ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.

Bila ya kufanya maamuzi hayo, bei za mafuta zingefikia kiwango cha juu cha Shilingi 2,638 kwa lita ya petroli (Dar es Salaam), Shilingi 2,648 kwa lita ya petroli (Tanga); na Shilingi 2,693 kwa lita ya petroli (Mtwara).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post