Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amefanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi kutoka mgodi wa Nyanzaga (Nyanzaga Mining Company Limited) uliopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza lengo ikiwa ni kupata mrejesho wa maandalizi ya awali kabla ya mgodi huo kuanza uzalishaji.
Dkt. Biteko amefanya mazungumzo hayo akiwa ziarani Kahama mkoani Shinyanga na kutumia fursa hiyo kueleza utayari wa Serikali kuweka mazingira rafiki kwa mgodi huo ikiwemo kufikisha huduma muhimu kama nishati ya umeme, maji na barabara ili kurahisisha shughuli kuanza.
Ujumbe huo kutoka mgodi wa Nyanzaga ukiongozwa na Meneja Mkuu, Damien Valent umemhakikishia Waziri Biteko kuwa maandalizi ya ufunguzi wa mgodi huo yanaendelea vyema ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya ardhi ili kuwalipa fidia wananchi watakaopisha shughuli za mgodi.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Afisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini Kahama Mhandisi Jeremiah Hango, Kamishna Msaidizi Wizara ya Madini Maruvuko Msechu, Kamishna Tume ya Madini Janeth Lekashingo, Afisa Mahusiano mgodi wa Nyanzaga Paul Gongo na Katibu wa mgodi huo Chelestino Malile.
Mgodi wa Nyanzaga ni miongoni mwa migodi minne iliyokabidhiwa leseni za uchimbaji madini mwezi Disemba mwaka jana katika hafla iliyoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo unatarajiwa kuendeshwa kwa ubia kupitia kampuni ya pamoja baina ya Serikali na mwekezaji iitwayo Sotta Mining Corporation Limited ambapo Serikali ina hisa za asilimia 16 na mwekezaji asilimia 84.
Na Mathias Canal na George Binagi, Kahama- Shinyanga
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko (kushoto) akizungumza na ujumbe kutoka mgodi wa Nyazanga ukiongozwa na Meneja Mkuu wa mgodi huo, Damien Valent (wa tatu kulia).
Viongozi kutoka mgodi wa Nyanzaga wakiongozwa na Meneja Mkuu wa mgodi huo, Damien Valent (kushoto), Afisa Mahusiano baina ya mgodi na Serikali Paul Gongo (katikati) na Katibu wa mgodi Chelestino Malile (kulia).
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Madini wakifuatilia kikao hicho. Kutoka kushoto ni Katibu wa Waziri wa Madini Mhandisi Kungulu Kasongi, Afisa Madini Mkazi Kahama Mhandisi Jeremia Hango, Kaimu Kamishna Wizara ya Madini Maruvuko Msechu na Kamishna Tume ya Madini Janeth Lekashingo.
Social Plugin