Picha Ikimuonesha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Daudi Kaali alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari hawapo katika picha, kuhusu matengenezo ya Mitambo, katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Umwagilijai Jijini Dodoma jana.
Picha ikionesha moja ya mtambo uliokarabatiwa unaotumika katika ujenzi wa skimu za kilimo cha umwagiliaji.
Mhandisi Hassan Dyali akizungumza na waandishi wa habari kuhuasiana na sehemu ya majukumu ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ya Ukarabati wa Mitambo inayotumika katika Ujenzi wa Skimu za Kilimo cha Umwagiliaji nchini.
**
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Kiasi cha fedha shilingi Bilioni Mbili za Kitanzania, zitatumika katika ukarabati na matengenezo ya mitambo inayotumika katika ujenzi wa miundombinu katika skimu za kilimo cha Umwagiliaji nchini.
Hayo yamesemwa jana jioni jijini Dodoma, na kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Daudi Kaali alipokuwa akizungumza waandishi wa habari katika viunga vya ofisi za Tume hiyo wakati zoezi la ukabati wa mitambo hiyo ukiendelea.
Bw. Kaali alisema nchi nzima ina mitambo zaidi ya 53 na inayoweza kutengenezwa ni mitambo 44 na malengo yaliyowekwa na Tume hiyo ni kutengeneza mitambo 43 hadi kufikia mwakani 2023. “Tutaokoa fedha nyingi kwani kukodi mtambo mmoja siyo chini ya Sh. Milioni moja kwa siku moja na unaweka kukuta, skimu moja inaweza ikahitaji siku hata ishirini au theathini kwa ajili ya matengenezo , hivyo kwa mahesabu ya haraka utaona ni fedha nyingi sana zinahitaji kukodisha mtambo mmoja kwa siku”. Alisisitiza Kaali.
Aidha alifafanua kuwa, Tume hiyo imetenga wastani wa hekta laki mbili na hamsini kwa mwaka zinazoweza kuendelezwa, hivyo matengenezo ya mitambo hiyo yataweza kuongeza kasi ya kuweza kuendeleza eneo hilo. “Tukienda hivi baada ya miaka mitano tunaweza kuwa tumeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kufikia hekta milioni moja na laki mbili. Alisema.
Mhandisi Hassan Ndyali, ni Msimamizi wa kitengo cha mitambo hiyo anafafanua kuwa, pamoja na kuwa kazi ya kukarabati mitambo hiyo ni sehemu ya majukumu ya ofisi, alisema kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe “Ambaye alitamani sana kuona tunafanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kukamilisha kwa wakati ili mitambo hiyo iweze kuleta tija kwa Taifa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji”,alisisitiza Mhandisi Ndyali.
Mmoja wa fundi wa mitambo hiyo Bw. Raphael Kanuha, amewahakikishia wakulima kuwa mashine hizo zitakamilika ndani ya muda mfupi na zitaingia kazini na kufanya kazi kwa ufanisi.