Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI WA DINI MWANZA WAKEMEA VITENDO VYA MAUAJI NCHINI


Viongozi wa Dini mkoani Mwanza wamekemea na wamelaani vikali matukio ya vitendo vya mauaji yanavyoripotiwa katika mikoa mbalimbali nchini na kuibua taharuki katika jamii ambapo wameitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kukomesha matukio hayo.

Viongozi hao wametoa kauli hiyo Januari 31, 2022 wakati wakizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza ambao pamoja na mambo mengine umelenga kutafuta mwarobaini wa kutokomeza matukio hayo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza Askofu Charles Sekela amesema matukio mengi ya mauaji yanayoripotiwa nchini chanzo chake ni mmomonyoko wa maadili katika jamii.


Askofu Sekela amesema viongozi wa dini wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanarejesha maadili na hali ya amani katika jamii na hivyo kutoa rai kwa Serikali kuwashirikisha viongozi hao katika kusaka suluhisho la vitendo hivyo vya mauaji.

“Chanzo cha mauaji haya ni wivu wa mapenzi, dhuruma na visasi katika jamii ambapo hayo yote anayeweza kuyatatua ni Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina dhamana ya kulinda maisha ya rai wake na mali zao hivyo tuwaombe sana viongozi wetu watimize wajibu wao” ameeleza Askofu Sekela akihimiza Serikali kupitia vyombo vyake kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kutokomeza vitendo hivyo", amesema.


Pia Askofu Sekela amesisitiza kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vitongozi na Mabalozi wa nyumba kumi wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wengine ili kuzuia vitendo vya mauaji kabla havijatokea kwani wao wako karibu na wanajamii.


Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke amewataka viongozi wenzake wa dini kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo na migogoro mbalimbali katika jamii badala ya kuwa sehemu ya migogoro hiyo.


“Tuwe sehemu ya kutatua matatizo kwani sisi ni grisi, tunatakiwa kulainisha vyuma na siyo kuwa sehemu ya kuchochea migogoro” ameleza Sheikh Kabeke huku akitoa rai kwa mamlaka mbalimbali za Serikali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na mabaraza ya Halmashari kuwashirika viongozi wa dini katika kutatua migogoto mbalimbali.


Awali akiwasilisha mada ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto KIVULINI, Yassin Ally amesema ripoti ya haki za binadamu inaonesha kuwa asilimia 71.8 ya vitendo vya mauaji vinavyoripotiwa chanzo chake ni wivu wa mapenzi na asilimia zinazobaki ni migogoro ya umiliki wa mali na hivyo kuhimiza wazazi, waalimu na viongozi wa dini kuongeza nguvu katika malezi ya watoto hatua itakayosaidia kupambana na vitendo hivyo.


Mkutano huo wa Viongozi wa Dini mkoani Mwanza umefikia jumla ya maazimio 17 ambayo wamesema yataboreshwa na kuwasilishwa katika ngazi mbalimbali ikiwemo serikalini kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji vilivyotishia amani katika siku za hivi karibuni.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza, Askofu Charles Sekela akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke akichangia hoja kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakinasa matukio wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI, Yassin Ally akichagiza mada wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI, Yassin Ally akichagiza mada wakati wa mkutano huo.
Mkutano wa Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza uliolenga kutafuta mwarobaini wa vitendo vya mauaji vinavyoripotiwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Mshauri wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la EAGT Kiloleli, Dkt. Jacob Mutashi akitoa ushauri wakati wa mkutano wa mkutano huo ambapo ameshauri maadili kwa watoto kuangaziwa ikiwemo Serikali kupiga marufuku mikusanyiko ya watoto isiyo na tija ikiwemo madisko 'disco toto'.
Mwenyekiti Mwenza Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Wilaya ya Ilemela, Mchungaji Elihuruma Swai akichangia mada kwenye mkutano huo.
Mchungaji wa Kanisa la PAG Busweli wilayani Ilemela, Mch. Upendo Isaya akichangia kwenye mkutano huo.
Katibu Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Mkoa Mwanza (JUWAKITA), Zainabu Huruma (kulia) akichangia hoja kwenye mkutano huo.
Viongozi wa dini mbalimbali mkoani Mwanza wakifuatilia mkutano huo.
Viongozi wa dini mkoani Mwanza wakiliombea Taifa pamoja na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni jitihada za kusaidia kuleta hali ya amani nchini.
Viongozi wa dini mkoani Mwanza wakiliombea Taifa.
Tazama Video hapa chini

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com