Mtafiti Mwandamizi kutoka Mamlaka ya afya ya mimea na udhibiti wa viatilifu Tanzania (TPHPA), Ramadhani Kilewa (kulia)akitoa mafunzo ya matumizi sahihi ya viatilifu.
Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
WAKULIMA wa Pamba, Mahindi na Mpunga zaidi ya 80 kutoka katika Mikoa 14 ya Tanzania Bara ikiwemo mikoa ya Kanda ya Ziwa Shinyanga, Simiyu, Mwanza na Geita wamepata mafunzo ya matumizi sahihi ya Viuatilifu.
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa muda wa wiki moja yaliyoendeshwa na wataalamu na watafiti wa visumbufu vya mimea waliyokutana na wakulima maafisa ugani na wasambazaji wa pembejeo za kilimo kutoka katika mamlaka ya afya ya mimea na udhibiti wa viuatilifu nchini TPHPA yenye makao makuu jijini Arusha.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Mamlaka ya afya ya mimea na udhibiti wa viatilifu Tanzania (TPHPA), Ramadhani Kilewa, ambapo zamani ilijulikana (TPRI), amesema wametoa mafunzo hayo ya viatilifu kwa wakulima zaidi ya 80 Kanda ya Ziwa ili wakawe mabalozi kwa wenzao na kukuza sekta ya kilimo.
Amesema kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wakulima, kuwa viatilifu vya siku hivi hafifanyika kazi na kushindwa kuuwa wadudu mashambani, lakini kumbe hawajui namna ya kuvitumia kwa usahihi, na kusababisha mazao yao kuendelea kushambuliwa na kukosa mavuno mengi.
“Mafunzo haya ya matumizi sahihi ya viuatilifu tumeyatoa kwa wakulima zaidi ya 80 kutoka Kanda ya Ziwa, ukiwamo mkoa wa Simiyu, Geita, Mwanza na wenyeji Shinyanga, ambayo yatakwenda kubadilisha dhana iliyojengeka kuwa vitalifu vya siku hizi ni feki, ambapo wakivitumia kama tulivyowafundisha watapata mavuno mengi,”alisema Kilewa.
Aidha Mkuu wa kitengo cha Mafunzo kwa wakulima na wauzaji wa Pembejeo kutoka TPHPA Jumanne Msalama, amesema mafunzo hayo yameendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya mimea namba 4 ya mwaka 2020, ambayo inamtaka kila mtu anayejihusisha na usambazaji wa viuatilifu apate mafunzo kabla ya kupata Leseni.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary, akizungumza kwenye mafunzo hayo, amewataka wakulima hao wakayatumie vizuri mafunzo waliyopata, pamoja na kufundisha wenzao namna ya matumizi sahihi ya viatilifu, ili wapate mavuno mengi na kukua kiuchumi.
Aidha, alitoa tahadhari kwa wafanyabiashara ambao husambaza ama kuuza Pembejeo za kilimo, wasiuze viatilifu feki ambavyo vimekuwa vikiwatia hasara wakulima, na kubainisha watakao kamatwa Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria.
Nao baadhi ya wakulima hao akiwamo Boniface Mbasa, walisema wanafurahi kupewa mafunzo hayo ya matumizi sahihi ya viatilifu, na kukiri ni kweli walikuwa wakikosea matumizi yake, ambapo walikuwa wakitumia kimazoea, huku wakiiomba Serikali idhibiti uingizwaji wa viatilifu feki hapa nchini.
Mafunzo kwa vitendo yakiendelea.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Zuwena Omary akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Mkuu wa kitengo cha Mafunzo kwa wakulima na wauzaji wa Pembejeo kutoka TPHPA Jumanne Msalama akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Shinyanga (Uchumi, Kilimo na Mifugo), Beda Chamatata akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Social Plugin