Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI KUPANDA MITI MILIONI 14 KUPITIA KAMPENI YA SOMA NA MTI

Waziri wa nchi,Ofisi ya Makamo wa Rais-Mazingira Seleman Jafo akimwagilia maji mti kwenye uzinduzi wa kampeni ya soma na mti inayolenga kutunza na kuongeza uhifadhi wa mazingira.

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog, DODOMA.

SERIKALI imesema imepanga kupanda miti zaidi ya milioni 14 kupitia wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo vikuu huku  ikiagiza maafisa mazingira nchini kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi sekondari na vyuo wanafanikisha jambo hilo kwa viwango vya juu ili kukabilianana mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yameelezwa leo Jijini hapa  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Seleman Jafo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na Vyuo nchini.

Waziri Jafo amesema wanafunzi waliopo katika shule za msingi na sekondari jumla wapo milioni 14.1 hivyo wamepanga kila mwanafunzi apande mti mmoja ili kufikisha idadi hiyo huku  kwa upande wa vyuo vya kati na vyuo vikuu kuna jumla ya wanafunzi 400,000 ambao nao wote watapanda miti.

“Lengo tunataka kila mwanafunzi wa shule ya msingi,sekondari na Chuo apande mti ,Wizara ya elimu hili liangalieni kupitia bodi ya mikopo maana ukame unazidi kuongezeka,”amesema.

Kadhalika Waziri Jafo ametumia fursa hiyo kuwaagiza Maafisa Mazingira Nchini kuisimamia ipasavyo kampeni hiyo kwa kwenda mashuleni na vyuoni kuikagua miti hiyo ambayo itakuwa imepandwa.

Vilevile,Waziri huyo amesema ukosefu wa mvua katika siku za hivi karibuni unasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa ikiwa ni pamoja na miti kupandwa.

“Ukiangalia Nchi yetu ukame umeongezeka mvua ilikuwa inaanza kunyesha kuanzia mwezi wa tisa lakini  leo tuna Jnauari lakini mvua haijaanza hii ni kutokana na mabadiliko ya Tabia nch,"amesema na kuongeza;

Lengo la kampeni hii ni kuhamasisha kila mwanafunzi kupanda miti ambapo  kila mwanafunzi nchini akipanda mti mmoja idadi ya miti itafikia milioni 14, hii itamfanya kila mwanafunzi kujivunia pindi atakapo hitimu masomo yake kwamba aliaacha alama ya mti shuleni ambayo inatunza mazingira,"amesema.

Vilevile amesema Kampeni hiyo ya upandaji miti katika  shule zote nchini inatekeleza  agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutokana na maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa ya kuhakikisha ajenda ya mazingira inatekelezwa kikamilifu na kuifafanua kuwa ajenda hiyo itakuwa  ya kudumu .

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Dodoma,Anthony Mtaka amewataka maafisa elimu kwenda kurudisha au kuanzisha klabu za mazingira mashuleni kwa sababu walengwa wakubwa wa kampeni hiyo ni wanafunzi hivyo ni rahisi kuendeleza kampeni hiyo kupitia klabu hizo mashuleni.

Pia amemuomba Waziri Jafo kusimamia  eneo la Mzakwe ambapo Makamo wa Rais ametembelea mara mbili lakini haliko vizuri hivyo kumuomba  kuagiza wataalamu  kwenda kulingalia kwa umakini eneo hilo.

Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,David Silinde ameziagiza Shule zote nchini kuhakikisha kampeni ya soma na mti inatekelezwa pamoja na kufufua na kuanzisha klabu zote za mazingira nchini.

"Hili siyo ombi ni lazima shule zote nchini zikafufue na kuanzisha klabu za mazingira,"amesema Silinde.
Waziri wa nchi,Ofisi ya Makamo wa Rais-Mazingira Seleman Jafo na wanafunzi wakipanda mti kwenye uzinduzi wa kampeni ya soma na mti inayolenga kutunza na kuongeza uhifadhi wa mazingira.
Waziri wa nchi,Ofisi ya Makamo wa Rais-Mazingira Seleman Jafo akiongea kwenye uzinduzi wa kampeni ya soma na mti inayolenga kutunza na kuongeza uhifadhi wa mazingira.
Naibu Waziri Tamisemi  Davis Silinde akiongea kwenye uzinduzi wa kampeni ya soma na mti


Baadhi ya wanafunzi walioshiriki uzinduzi wa kampeni ya soma na mti wakisikikiza kwa makini hotuba za Viongozi kuhusu masuala ya mazingira

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com