Polisi katika jimbo la Zamfara kaskazini-magharibi mwa Nigeria wanasema wamewakamata watu wanne wanaodaiwa kuhusika na ulaji nyama za watu na kuuza sehemu za binadamu- jambo ambalo ni nadra sana katika eneo hilo.
Kamishna wa polisi katika jimbo hilo Ayuba Elkanah aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Gusau siku ya Alhamisi kwamba washukiwa hao walikamatwa baada ya maafisa wa upelelezi kupata maiti katika jengo ambalo halijakamilika huku baadhi ya sehemu za mwili zikiwa zimetolewa.
Ilikuwa ni katika harakati za kufanya uchunguzi wa kupotea kwa mvulana wa miaka tisa. Washukiwa hao wakiwemo wanaume wawili na wavulana wawili walikamatwa wiki iliyopita, kulingana na mkuu wa polisi, na kwamba washukiwa wengine wa genge hilo wanasakwa.
Mkuu huyo wa polisi alisema hadi sasa uchunguzi umebaini kuwa mara mbili kiongozi wa genge hilo aliwalipa washukiwa wengine watatu kiasi cha Naira Laki Tano (sawa na $1,207) kwa ajili ya sehemu za binadamu.
Kuhusika na uuzaji wa sehemu za binadamu na ulaji nyama si jambo la kawaida katika jimbo la Zamfara. Lakini ni moja wapo ya maeneo ya Nigeria yaliyokumbwa zaidi na wimbi la mauaji na utekaji nyara kwa ajili ya fidia na magenge yenye silaha huku mamlaka zikikabiliwa na ukosoaji kwa kushindwa kukabiliana na ghasia hizo.
Hata hivyo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Alhamisi kamishna wa polisi Ayuba Elkanah alisema vikosi vya usalama pia vimewaokoa watu kumi na saba waliotekwa nyara hapo awali kutoka jimbo jirani la Niger na kupelekwa Zamfara.
Alisema vikosi vya usalama vilivyokuwa kwenye doria pia vimefanikiwa kupata baadhi ya silaha ikiwa ni pamoja na vifaa vya kurusha roketi kutoka kwa genge moja baada ya makabiliano ya risasi karibu na msitu.
Wiki iliyopita, takriban watu 200 waliripotiwa kuuawa wakati wa msururu wa uvamizi katika vijiji kadhaa jimboni humo.
Chanzo - BBC Swahili
Social Plugin