Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika kikao cha wataalam wa Sekta ya Uvuvi (hawapo pichani) kilichojadili hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo amewaeleza wataalam hao kuwa katika kipindi kilichobaki cha mwaka wa fedha 2021/2022 ni lazima lengo la kukusanya bilioni 40 litimizwe. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi akizungumza wakati wa kikao cha wataalam wa sekta ya uvuvi kilichojadili kuhusu ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. Kulia kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma.
Mhasibu Mkuu wa Sekta ya Uvuvi, Bw. Lupakisyo Mwakitalima (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwenye sekta ya uvuvi kwenye kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi na wataalam wa sekta hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Morena Hotel Jijini Dodoma.
Baadhi ya Viongozi na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu ukusanyaji wa maduhuli kwenye sekta hiyo.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na Wataalam wa Sekta ya Uvuvi waliofanya vizuri katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo wote wamekusanya zaidi ya asilimia 70 ya lengo walilopangiwa. Kulia waliokaa ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala.
...............................................................
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wataalam wa sekta ya Uvuvi kuhakikisha wanakusanya maduhuli ya serikali ili kutimiza lengo la kukusanya bilioni 40 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (15.01.2022) kwenye kikao cha wataalam wa sekta ya uvuvi kilichojadili hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia sekta ya uvuvi ambapo mpaka sasa sekta hiyo imekusanya bilioni 10 kati ya bilioni 40 zilizolengwa.
Katika kikao hicho taarifa za ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ziliwasilishwa kwa kila kituo ambapo pia changamoto ziliwasilishwa na kujadiliwa namna gani ya kuweza kukabiliana nazo ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhili unafikia malengo yaliyowekwa.
Akizungumza na wataalam hao Waziri Ndaki amesema kuwa ni lazima wataalam kuhakikisha wanaongeza usimamizi kwenye maeneo yao ili malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yatimie. Ili kuhakikisha malengo ya ukusanyaji maduhuli yanafikiwa Waziri Ndaki amesema vituo vitatakiwa kutoa taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli kila wiki ili kama kunakuwepo na changamoto iweze kutatuliwa kwa wakati.
Lakini pia wataalam wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kwa kujitolea ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yanatimizwa. Waziri Ndaki amewaeleza wataalam hao kuwa katika muda wao wa utumishi ndani ya sekta ya uvuvi ni lazima waache alama ikiwemo ya ukusanyaji mzuri wa maduhuli.
Wataalam hao wametakiwa kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuhakikisha wanasimamia sheria, kanuni, miongozo na taatibu zilizowekwa. Pia wametakiwa kuhakikisha kuwa wanalinda na kuzisimamia rasilimali za uvuvi. Vilevile amewaonya wataalam hao kutojihusisha na uvuvi haramu kwani wakibainika hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Waziri Ndaki amesema kuwa wizara ina malengo makubwa ya kuwawezesha wavuvi ili wakue kimapato na hivyo waweze kuchangia kwenye pato la taifa kupitia sekta ya uvuvi. Aidha, amesema kuwa wizara itafanya mapitio ya tozo mbalimbali za uvuvi na kuzifanyia marekebisho endapo yatahitajika.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi amesema kuwa lengo la kuitisha kikao hicho ni kufanya tathmini ya hatua iliyofikiwa katika ukusanyaji maduhuli ya serikali pamoja na hali ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi.
Pia amemshukuru Waziri kwa uamuzi wake wa kuitisha kikao hicho kwani kimesaidia kwa kuwawezesha wakuu wa vituo vyote Tanzania kukaa kwa pamoja kujadili changamoto walizonazo na kutoka na mkakati wa pamoja ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhuli unakwenda vizuri.
Getrude Migodela kutoka Kitengo cha Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi Mwanza amesema kuwa watakwenda kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kuhakikisha wanakusanya maduhuli kulingana na malengo yaliyowekwa. Pia ameishikuru Wizara kwa maelekezo yake ya kuwataka wafanyabiashara wa samaki na mazao ya uvuvi waanze kulipia kwenye eneo mzigo unapotoka kwa kuwa hiyo itawasaidia kuongeza mapato kwenye vituo vyao.
Kikao hicho cha wataalam kimefanyika kwa lengo la kuwakutanisha wataalam wa uvuvi wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili waweze kujadili changamoto na mikakati itakayowezesha sekta ya uvuvi kutimiza malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali lakini pia kuhakikisha uvuvi haramu unadhibitiwa.