Katibu wa kikundi cha wanawake Buwea Apolina Beda akionesha bidhaa zinazotokana na soya yakiwemo maziwa ya soya na Unga. Picha na Alodia Dominick
Katibu wa kikundi cha wanawake Buwea Apolina Beda akionesha bidhaa zinazotokana na soya yakiwemo maziwa ya soya na Unga.
Na Alodia Dominick, Bukoba.
Wazazi na walezi mkoani Kagera wametakiwa kutumia unga wa soya katika vyakula vya watoto kutokana na unga huo kumjenga kiafya mtoto na hivyo kukua akiwa na afya njema na mwenye akili.
Katibu wa kikundi cha maendeleo ya wanawake kilichopo manispaa ya Bukoba cha Bukoba Women Empowerment Association (BUWEA) Apolina Beda amesema, wazazi na walezi watumie unga wa soya na maziwa yanayozalishwa katika kiwanda cha kikundi hicho kuzijenga afya za watoto wao kutokana na unga wa soya kuwa na protini nyingi sawa na nyama.
Amesema mtoto chini ya miaka nane anapotumia unga wa soya unamjenga kimwili na kiakiri hivyo kumuwekea kinga ya kutougua maradhi ya mara kwa mara na kumsaidia kukua akiwa na afya njema.
Beda amesema kutokana na mkoa wa Kagera kuwa na kiwango cha udumavu kwa watoto kikundi chao kilikuja na suruhisho la kuanzisha kiwanda cha kutengeneza maziwa ya soya na kusindika unga lengo likiwa ni kujenga afya bora kwa watoto kwa kuhamasisha wazazi na walezi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikundi cha Buwea Regina Majaliwa ameeleza kwamba, kikundi hicho ni mwavuli wa vikundi 138 vyenye wana chama 1,280 ambavyo vinajishughulisha na shughuli za ujasiliamali, kilimo, ufugaji na uzalishaji wa maziwa ya soya na unga wa soya.
Majaliwa ameeleza kwamba, kiwanda chao kinazalisha maziwa ya soya kati ya lita 200 hadi 300 kwa mwezi kutokana na watu wanaohitaji lakini mashine zina uwezo wa kuzalisha lita 100 hadi 200 kwa siku hivyo akaomba jamii ya mkoa wa Kagera na mikoa mingine kutumia bidhaa yao kwani ni dawa tiba kwa watoto na kwa watu wa rika zote wakiwemo wazee.
Amesema walizitembelea shule za msingi zilizopo manispaa ya Bukoba na kuwashauri walimu wa lishe wanunue unga huo kwa ajili ya kuchanganya kwenye uji wa watoto wanapopikiwa shuleni ingawa amesema bado hawajatumia unga huo richa ya kuhamasisha.
Mmoja wa wanakikundi Alisia Gaudini ambaye anajihusisha na kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa kuku amesema kuwa, Buwea imemsaidia kumpatia elimu ya ujasiliamali ni pamoja na kumuelimisha jinsi ya kuwalea watoto wake kwa kuwapatia vyakula bora vya kujenga mwili ikiwemo matumizi ya unga wa soya.
Gaudini amesema jamii inapaswa kuhamasika kutumia vyakula walivyonavyo kwa ajili ya kujenga lishe bora ya watoto wao kwani mtoto anapokuwa na afya njema hata anapofikia rika la utu uzima inamfanya aweze kuwa na akili ya kujua kuchanganua mambo tofauti na mtoto aliyedumaa hata utu uzima akili inakuwa imedumaa.
"Tuwapatie chakula bora watoto wetu wakue kiafya na kiakiri ili tupate viongozi bora wa miaka ijayo, lishe bora ni kinga ya magonjwa tutumie vyakula mchangayiko na unga wa soya kwani umedhibitika una protini nyingi" Amesema Gaudini
Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera unakabiriwa na kiwango cha udumavu asilimia 37 kwa mwaka 2020/2021.
Social Plugin