WAZIRI MKUU AVUTIWA KASI YA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapongeza Wakuu wote wa Mikoa na Wakuu wote wa Wilaya nchini kwa kazi nzuri waliyofanya ya kusimamia miradi ya maendeleo na hasa ujenzi wa madarasa.

“Kupitia kwako Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya waliopo hapa, nitoe pongezi kwa Wakuu wengine wa Mikoa na Wilaya kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya maendeleo. Hii ni pamoja na usimamizi wa fedha, uratibu wa matumizi ya fedha hizo na usimamizi wa kuhakikisha miradi inakuwa ya viwango,” amesema.

Ametoa pongezi hizo leo mchana (Jumapili, Januari 02, 2022) wakati akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali wa mkoa wa Ruvuma kwenye uwanja wa ndege wa Ruhuwiko, wilayani Songea mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo.

Waziri Mkuu amesema amefanya ziara kwenye mikoa ya Mbeya, Lindi, Dodoma, Dar es Salaam na sasa yuko Ruvuma na amejionea kazi nzuri iliyofanyika. Amesema ifikapo Januari 5, usafi ufanyike kwenye madarasa yaliyojengwa ili yakabidhiwe kwa Wakuu wa Shule.

“Ari ya usimamizi wa ujenzi iliyooneshwa katika miradi hii, ikifanyika kwenye miradi mingine yote, ni lazima nchi hii itafika mbali. Tunatambua katika miradi mikubwa kama hii hapakosi changamoto, lakini kuna wengine ambao wamefanya kazi nzuri hadi kubakiza fedha.”

Amewataka wasimamie miradi iliyosalia ya afya, maji na ujenzi wa barabara (TARURA) kwa mtindo huohuo. Ametumia fursa hiyo kumwahidi Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Bw. Oddo Mwisho kwa niaba ya wenzake, kwamba Serikali itasimamia vizuri miradi mingine kama ilivyosimamia miradi hii ya maendeleo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema siyo sahihi kuiita miradi inayotekelezwa hivi sasa kuwa ni ya UVIKO 19 bali ni miradi ya Maendeleo ya Kitaifa ambayo inatokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Hii miradi ni ya maendeleo ya Kitaifa lakini imetokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ilielekeza madarasa yajengwe kwa haraka ili kukabiliana na uhaba wa madarasa wa kila mwaka. Kupatikana kwa hizi fedha za mkopo wenye masharti nafuu ni ubunifu wa Mheshimiwa Rais wetu ili ziweze kukamilisha na miradi mingine kwenye elimu, afya, maji na barabara za vijijini.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nchini wawahimize wananchi kwenye maeneo yao watunze akiba ya chakula walichonacho na wapunguze kukiuza.

“Wakuu wa Mikoa na Wilaya kaeni na wananchi na kuwasisitiza wahifadhi chakula na wapunguze kuuza ili kujiwekea akiba. Kama kuna mbegu za muda mfupi ni vema wahimizwe kuzitumia ili waweze kuzalisha chakula kingine ndani ya muda mfupi. Tuendelee kuwatia moyo wananchi wetu, tushirikiane pia na viongozi wa dini ili tumuombe Mungu atushushie mvua za kutusaidia tupate mazao,” amesema.

Ili kurejesha uoto wa asili ndani ya miaka mitatu hadi minne ijayo, amewataka wawahimize wananchi kupanda miti pindi mvua zikianza. “Tukirejesha misitu midogo midogo, hali ya unyevu na uchepechepe itarejea haraka. Tunapaswa pia kukemea tabia ya kukata miti hovyo,” amesisitiza.

“Tumeanza kushuhudia ukame uliopitiliza kwenye mikoa hii ya Kusini. Kwa kawaida mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini imekuwa ikitumika kutoa akiba ya chakula kwa mikoa mingine, kwa hiyo tunapaswa tukabiliane na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwahamasisha wananchi wapande miti kila mahali.”

Mapema, Mkuu wa Mkoa huo, Brig. Jenerali (Balozi) Wilbert Ibuge alimweleza Waziri Mkuu kuwa mkoa huo ulipokea sh. bilioni 10.24 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 500 na mabweni matatu kwa ajili ya shule zenye mahitaji maalum.

“Kwa sasa, ujenzi wa madarasa yote 500 umekamilika kwa asilimia 100 na ujenzi wa mabweni haya matatu unaendelea vizuri isipokuwa wamefikia hatua ya maboma. Tunaahidi kuwa yatakamilika kabla shule hazijafunguliwa,” alisema.

Alisema kwenye sekta ya afya, walipokea sh. bilioni 22.75 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye tarafa 11 ambazo hazikuwa na vituo vya afya kabisa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post