RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Sita inataka kuanzisha viwanda vya kutengeneza chanjo ya virusi vya corona ikiwa ni sehemu ya mipango ya kukabili ugonjwa wa Covid-19 na magonjwa mengine.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus imeeleza kuwa, Rais Samia alisema hayo jana jijini Brussels nchini Ubelgiji alipokutana na kuzungumza na Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel.
Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa, Rais Samia alimweleza Michel kuwa Tanzania ina lengo la kutengeneza kinga za kuokoa maisha kwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC).
Rais Samia yupo Ubelgiji kwa ziara rasmi kwa mwaliko wa Michel na alisema hadi mwaka 2030 Tanzania huenda itatumia Sh bilioni 216 kuagiza kinga za magonjwa.
Alisema anatarajia ataungwa mkono kutekeleza lengo la kuzalisha kinga kwa kuwa ana imani katika lengo hilo na mradi huo ukitekelezwa Tanzania itafungua milango zaidi kuimarisha ushirikiano na Ulaya.
Wakati huohuo, Rais Samia alitoa mwito kwa Umoja wa Ulaya (EU) kuendelea kuisaidia serikali ya Burundi na akasema umoja huo una jukumu muhimu kwa maendeleo na uimara wa nchi hiyo.
“Burundi tulivu ni muhimu kwa Ukanda wa Maziwa Makuu, muhimu pia kwa EU na muhimu kwa dunia,” alisema Rais Samia.
Tangu kuanzishwa kwa ushirikiano rasmi na EU mwaka 1975, Tanzania imepokea msaada wa maendeleo wenye thamani ya zaidi ya Euro bilioni 2.3 ambazo ni sawa na Sh trilioni 5.98.
Social Plugin