Mwanafunzi wa Shule ya Gremon Education Center eneo la Bamburi, kaunti ya Mombasa nchini Kenya anauguza majeraha mabaya katika Hospitali ya Rufaa ya Coast General baada ya kudaiwa kupokezwa kichapo cha mbwa koko na mwalimu mkuu kwa kula chapati zake.
Mama yake mwanafunzi huyo, Agnes Ngure alisema kuwa mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 15, anapokea matibabu ya figo hospitalini humo baada ya kujeuriwa vibaya na mwalimu mkuu wa shule hiyo Nancy Geshew na wanafunzi wenzake.
Kulingana na mama huyo, mwanawe aliadhibiwa na mwalimu mkuu kwanza kabla ya kumkabidhi kwa wanafunzi wenzake na kuwaelekeza wamwadhibu.
"Walioshuhudia tukio hilo wanadai kuwa mwalimu huyo alimvamia mwanangu kabla ya kumkabidhi kwa wanafunzi wenzake ambao walimpiga kwa njia ambayo imetajwa kuwa haki ya kundi," alisema.
Mwanafunzi huyo anashtumiwa kula chapati mbili ambazo zilikuwa zimetengewa mwalimu mkuu wa shule hiyo, K24 yaripoti.
Ngure pia aliongeza kuwa mwanawe alitengwa katika bweni la shule hilo bila kupewa matibabu na wazazi wake walijuzwa tu baada ya hali yake kuanza kudorora.
"Aliwekwa ndani ya bweni tangu Januari 23 na nilijulishwa hali yake jana (Januari 31) nilipoambiwa niende kumchukua mwanangu ambaye walidai alipata majeraha baada ya kutumia maji ya moto kuoga. Muda wote huo walikuwa wamemweka kitandani huku wakitumia chumvi, maji moto kuponya majeraha yake,” Ngure alisema.
Kisa hicho kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Kazadani huku Kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Nyali, Ibrahim Dafar akithibitisha kwamba mwalimu mkuu huyo amekamatwa. Dafar alisema wanasubiri ripoti ya p3 kabla ya mwalimu huyo kufikishwa kortini Jumatano, Januari 2.
Kamanda huyo wa polisi pia alifichua kuwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne ambaye aliongoza kundi lililompiga mwenzao anasakwa baada ya kuingia mafichoni.