Sehemu ya wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi
Na Dinna Maningo, Musoma
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua kadi mpya za wanachama za mfumo wa kielektroniki zenye taarifa na kumbukumbu muhimu huku akisema kuwa fedha zilizochangwa katika matembezi ya wanachama,Milioni 300 zitatumika kutengeneza kadi.
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa ameyasema hayo leo wakati wa hotuba yake katika kilele cha kusherekea miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi Februari, 5,1977 zilizofanyika leo Februari 5,2022 katika uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara, zilizohudhuriwa na wanachama kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na wananchi.
"Tulianza matembezi ya wanachama saa 12 asubuhi milioni 300 zimekusanywa zitatengeneza kadi za chama za kielectroniki, nawashukuru kwa kufanikisha sherehe za matembezi" ,amesema Mwenyekiti Samia.
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa amesema kuwa safari ya miaka 45 haikuwa nyepesi kwa sababu kulikuwa na ushindani na vyama vingine huku akitaja baadhi ya mafanikio ya chama hicho.
Samia amesema kuwa chama hicho kimeendelea kuongoza ambapo ushindi wa chama hicho unatokana na CCM kujenga imani na hivyo kuaminiwa na watu kutokana na misingi mizuri ya chama hicho.
Amesema kuwa katika miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM chama kimefanikiwa kuongeza mishahara kwa watumishi wake kwa asilimia 89 hadi 25 na kulipa madeni ambayo bado yataendelea kulipwa.
"TOT nao wamewekwa vizuri na ajira yao ni safi,mishahara imepanda kwa kiwango cha asilimia 89 hadi 25,CCM imekumbana na changamoto na kimekuwa na mageuzi ya mwelekeo ya kisera,miongozo hata mageuzi ya kimfumo" amesema.
Akizungumzia mafanikio yaliyofanywa na Serikali amesema kuwa miradi yote ya kimkakati itakamilishwa,kukamilisha miundombinu ya ujenzi ikiwemo ya usafiri na usafirishaji,nyumba za walimu ambapo tayali mafanikio yameonekana katika sekta ya afya,elimu,maji,kilimo na mifugo ambapo pembe jezo za kilimo zimetolewa bure kwa baadhi ya wakulima.
"Tumeweza kudhibiti janga la Corona (ugonjwa wa Uviko 19) na watu kuoata chanjo,sekta ya usafiri na usafirishaji imehimarika mafanikio mengi yameonekana hata mkoa wa Mara",amesema.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ili kuwatumikia wananchi,ametoa wito kuhimarishwa kwa ulinzi na usalama kwa kuepuka vitendo vitakavyohatarisha amani ya nchi kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Taifa,Daniel Chongolo amesema kuwa wakati chama cha CCM kimeanzishwa kulikuwa na wanachama 500,000 lakini hadi sasa kina wanachama milioni 12.
Chongolo amesema kuwa katika kuhakikusha chama kinaendelea kuhimarika kiliadhimia uundwaji wa kadi za chama za kielektroniki na hadi leo wanachama waliosajiliwa kwenye mfumo huo ni zaidi ya milioni mbili.
Ametoa wito kwa watendaji wa CCM kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kazi inakamilishwa kwa wakati katika zoezi la usajili wa kadi za hizo.
Katibu wa halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Itikadi na uenezi,Shaka Hamdu amempongeza Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuwa ndiye alichangia kuhakikisha mfumo huo unakuwa vizuri.
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara,Samwel Kiboye (Namba 3) ameupongeza uongozi wa chama Taifa na Chama mkoani Mara na Serikali ya Mara kwa maandalizi mazuri ya sherehe hiyo.
Kiboye amemuomba Samia kutoogopa kuwaondoa viongozi wabovu huku akilalamikia moja ya wilaya mkoani Mara kujenga madarasa chini ya kiwango huku miundombinu ya barabara ikijengwa kwa kasi ndogo.