BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) limeiagiza Halmashauri ya Mji wa Kibaha kufanya tathimini ya athari za kimazingira katika bonde la Ruvu kwa lengo la kuepusha athari zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu katika eneo hilo zikiwemo za ujenzi.
Aidha NEMC imeendelea kuwasisitiza wakuu wa mikoa yote nchini, kuendelea kusimamia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango waliotoa agizo la kulindwa mazingira katika maeneo yao yakiwemo ya vyanzo vya maji kwa ajili ya kuepusha athari zinazoweza kusababishwa kutokana na kukauka kwake.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo Dk. Samuel Gwamaka aliyasema hayo mara baada ya kutembelea baadhi ya maeneo ya bonde kwa lengo la kujionea hali halisi ya uhifadhi sambamba na kufanya tathimini ya baadhi ya maeneo ambayo halmashauri ya Mji wa Kibaha ilikusudia kufanya ujenzi wa shule.
"Nimekagua maeneo mbalimbali ya bonde hili na kubaini kuwa kuna athari nyingi za uharibifu wa kimazingira, sote tunatambua kuwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani mategemeo yao wote ya maji ni kutoka katika bonde hivyo tunapaswa kulitunza kwa nguvu zote", alisema Dk. Gwamaka.
Alisema changamoto inayojitokeza kwa Halmashauri ya Kibaha ni kuyachagua maeneo ni oevu ambayo pia ni vyanzo kwa ajili ya kujenga shule hizo, jambo ambalo kimsingi Mkurugenzi huyo alisema haliwezekani na Halmashauri hiyo inafapaswa kufanya tathimin upya.
"Wote tunajua kuwa maji yanatoka katika milima hasa kipindi cha mvua, sehemu ambayo ni hifadhi yake hata kama kuna mafuriko ni maeneo kama haya ambayo kama yasipotunzwa athari zake ni kubwa kubwa changamoto inayojitokeza ni msukumo wa maendeleo kama ilivyo kwa Kibaha ambayo inataka kujenga shule ndani hayo jambo ambalo ni hatari kwa mazingira haya" alisisitiza Dk. Gwamaka
Alisema hata jengo la Halmashauri ya Mji huo limejengwa katika eneo Oevu hali iliyolifanya likabiliwa na changamoto katika mifumo yake ya maji taka huku akisisitiza kwa wadau wote wakiwemo wawekezaji kusubiri ripoti ya athari za kimazingira katika eneo hilo kabla ya kufanya ujenzi wowote.
Mbali na hilo Mkurugenzi huyo alisema pia ujenzi wa kituo cha kuuzia mafuta katika eneo jirani na kambi ya JKT Ruvu unapaswa kusitishwa kwa kuwa utaathiri vyanzo vya maji kutokana na matangi yatakayowekwa ardhini ambayo yanaweza kusababisha mafuta kuvuja na hivyo kuathiri vyanzo vya maji.
Aliwataka wadau wote wa kimaendeleo kusubiri ripoti ya tathimini ya kimkakati inayofanyiwa kazi na Ofisi ya Rais ambayo itatoa majibu kuwa kama eneo hilo linafaa kwa ujenzi wa makazi au viwanda katika bonde hilo la Ruvu.
Awali Afisa Mazingira wa Halmashauri wa Mji wa Kibaha Maximilian Mtobu alisema wao kama taasisi ya Serikali wameupokea maagizo ya NEMC kwa umakini mkubwa kwa kuwa ndiyo taasisi inayotambua athari za kimazingira nchini yakiwemo maeneo ambayo walikusudia kufanya ujenzi huo
Alisema baada ya tathimini iliyofanywa na Baraza hilo ambayo imepinga ujenzi wa shule katika maeneo waliyokuwa wamekuusudia, watakaa na kujadili ili kuangalia ni wapi watafanya ujenzi huo ili pamoja na mambo mengine kuufanya ujenzi huo kuwa wa kudumu na wenye manufaa kwa Taifa.
Social Plugin