DKT. MPANGO AZINDUA SERA YA TAIFA YA MAZINGIRA,ATAKA KUWA ENDELEVU

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 blog-  DODOMA.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango amezinduzi sera ya taifa ya mazingira ya mwaka 2021 huku akielekeza zoezi hilo kuwa endelevu hadi nchi nzima itakapokuwa ya kijani.

Dkt. Mpango amezindua kampeni hiyo Jana Jijini hapa kwa kuongoza zoezi la upanda miti Jijini Dodoma katika maeneo ya  Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuelekea barabara ya Dodoma Dar es Salaam na kutumia nafasi hiyo  kuwataka Watanzania kuiendeleza na kuitunza ili kurejesha hali ya asili ya mazingira kwa vizazi vijavyo.

Akiongea kwenye uzinduzi huo alisema sera hiyo mpya imezingatia changamoto mpya za kimazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea duniani.

"Tunataka kuibadilisha nchi kuwa ya kijani kwa kurejesha hali ya asili ya mazingira iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu kazima zoezi la upandaji miti kuwa endelevu na shughuli za usafi wa mazingira zitakazo boresha afya ya jamii na elimu ya utenganishaji taka kwa ajili ya udhibiti wa taka ngumu,hili linawezekana,"alisema. 

Kadhalika Dkt. Mpango amesema suala la utunzaji wa Mazingira lisiwe kwenye matamshi bali linapaswa kufanywa kwa vitendo huku akiwaagiza wasimamizi wa mazingira kuwa wakali.

Katika Hatua nyingine Dkt. Philip Mpango ametoa siku 30  kwa Ofisi ya makamu wa Rais ,Muungano na Mazingira,Ofisi ya Rais TAMISEMI na ofisi ya mkoa wa Dodoma kuja na mpango mkakati wa kujanikisha Dodoma pamoja na kuja na sera na mpango mkakati kwa lugha ya Kiswahili.

 “Mheshimiwa Waziri Jafo uniletee na  huo mpango mkakati na uwe wa kihalisia uniletee kila baada ya miezi mitatu sasa kwenye hili pale utekelezaji utakapotokea unalega lega natoa tahadhari wahusika wote wawajibike wenyewe kabla sijaingilia kati natumaini wamenisikia.

“Mfanye hivyo zoezi liwe endelevu na nataka niupate mpango huu ndani ya miezi mitatu tunataka Dodoma iwe kama Singapore lazima Dodoma iwe ya kijani lazima Dodoma iwe safi,”amesema.

Aidha amewataka Mawaziri wa Kilimo,Maliasili na Utalii,Maji,Mifugo na Uvuvi pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara na Mazingira  kwenda kufanya tathmini na kumpa majibu hatua walizochukua katika ujenzi wa   bwawa la  Mwalimu Nyerere.

Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira, Seleman Jafo amesema awali kulikuwa na sera ya mwaka 1997 ambayo ilipata mafanikio makubwa na kuzalisha sheria  namba 20 ya mwaka 2004 na kanuni zake.

Amesema kwa kuwa Sasa kwa sasa  kuna mahitaji makubwa na matakwa mbalimbali ilisababisha waunde  sera mpya ya mazingiraa ambayo imezinduliwa leo.

Amesema Juni 5 mwaka 2021,wakati Makamu wa Rais akizindua kampeni kabambe ya mazingira  alitoa maelekezo ambayo ni pamoja na kuhakikisha sera ya mazingira inakamilika.

Amesema kwa kupitia sera hiyo Tanzania inaenda kuwa sehemu salama katika suala la mazingira na kuungana na mataifa mengine.

“Sera hii itaenda kuongeza fursa za jinsi gani urejeshaji wa taka unaweza kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja ama vikundi mbalimbali hili ni jambo ambalo lipo katika sera yetu jinsi gani tutatumia mbinu mbadala taka zinarejeshwa,”amesema.

Amesema sera hiyo  itaenda kuakisi hasa mabadiliko ya tabia nchi ambapo amemhakikishia Makamu wa Rais kwamba imezingatia   Mpango wa Taifa wa miaka mitano 2020-21mpaka 2025-2026 mpango endelevu wa mwaka  2030 na mpango ule wa  miaka 15 ulioanza mwaka  2011-2012 mpaka  2025-2026.

“Imani yetu mchakato wa sera hii utaenda kutekeleza masuala mbalimbali ambayo yataliokoa taifa letu hili na maelekezo yako ambayo umeyatoa muda wote kuhakikisha mazingira tunayatunza na tunayalinda kwa nguvu zote,”amesema.  

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinazingatia kampeni zote zilizopo zinazohisu mazingira ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wake kikamilifu.

Amesema,ili kuendana na hali ya ustawishaji Serikali  inatekeleza mkakati wa Taifa wa kupanda zaidi ya miti milioni 270 ambapo kila Halmashauri ina jukumu la kupanda miti milioni 1.5 ikiwemo ya kivuli na ya matunda.

Amesema kwa sasa dunia inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi hivyo ni wakati muafaka wa kuhakikisha kuwa lengo la kupanda idadi hiyo ya miti linafikiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema wamekubaliana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) kupanda  miti pembezoni mwa barabara ikiwemo katika ujenzi wa barabara za mzunguko wa nje katika Jiji la Dodoma.

Pia amesema wamekubaliana na Jiji la Dodoma kila mwenye kiwanja apande miti mitano mitatu ya matunda na miwili ya vivuli.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akipanda mti wakati alipo ongoza zoezi la upanda miti Jijini Dodoma katika maeneo ya  Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuelekea barabara ya Dodoma Dar es Salaam ikiwa ni siku ya uzinduzi wa sera ya taifa ya mazingira ya mwaka 2021 na kutumia nafasi hiyo  kuwataka Watanzania kuiendeleza na kuitunza ili kurejesha hali ya asili ya mazingira kwa vizazi vijavyo.




 Sehemu ya matukio katika picha kati ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango  akiwa na viongozi mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Sera  ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 leo Februari 12,2022 jijini Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post