MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Pololet Mgema amewataka wahitimu walioshiriki mafunzo ya wadau walioko kwenye sekta ya Utalii yaliyokuwa yakitolewa kwa siku tano na Chuo Cha Taifa cha Utalii kutumia vema mafunzo hayo ili kuleta ufanisi katika kazi zao.
Amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi ambapo Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inachukua hatua za kukabiliana na janga la UVIKO 19 kwa kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo kutoa fedha kuwezesha mafunzo hayo.
MKuu wa Wilaya huyo ameasema hayo wakati wa kufunga rasmi mafunzo ya UVIKO 19 kwa wadau wa Sekta ya Utalii yaliyofanyika kwa siku tano Songea Mkoani Ruvuma, ikijumuisha washiriki kutoka katika Wilaya zote za Mkoa huo.
"Mafunzo haya yakawape hamasa na fursa ya kuibua na kutangaza vivutio vilivyosahaulika kwenye Mkoa wetu wa Ruvuma ili mwisho wa siku viendelee kuwa na tija kwa Taifa kwa kuinua mapato ya nchi na mtu mmoja mmoja" amesema Mgema.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Utawala wa Chuo cha Taifa cha Utalii CPA Munguabella Kakulima akizungumza wakati wa hotuba ya utangulizi kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Shogo Mlozi Sedoyeka, amesema kuwa mafunzo hayo yataenda kuboresha Sekta ya Utalii na kwamba kufungwa kwa mafunzo hayo katika Mkoa wa Ruvuma kunatoa fursa kwa mikoa mingine kupata mafunzo hayo ambayo ni mikoa ya Iringa na Mbeya.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufadhili mafunzo hayo ambayo yanakwenda kuikomboa Sekta ya Utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
Mafunzo hayo yanalenga kusaidia Sekta ya Utalii kwa kuhakikisha kila mdau anapata uelewa sahihi wa namna ya kukabiliana na janga la UVIKO 19.
Mwisho.
Social Plugin